Kila mtu ambaye aikuwa akiziangalia taarifa
zile katika vyombo mbalimbali vya habari hakuonekana kushtuka sana kutokana na
kufahamu kwamba kuna siku kitu kama kile kingetokea kutokana na Katie kuwa
miongoni mwa watu ambao waikuwa wakiigiza filamu za ngono duniani.
Kila kitu
kilionekana kubadilika sana katika maisha ya Katie, mwanaume ambaye alikuwa
akimheshimu sana, Gibson kwa wakati huo hakuwa pamojanae. Katie akawa mwanamke
wa kulia tu, kila siku alikuwa akijifungia chumbani kwake na kulia kupita
kawaida.
Moyo wake ulikuwa ukimuuma kupita kawaida. Kuna wakati alikuwa
akijuta sababu zilizompelekea kuolewa na mwaname ambaye wala hakuwa amekaa nae
sana katika mahusiano huku wakati mwingine akijuta sababu ambazo zilimpelekea
kutokumwambia Gibson ukweli juu ya kazi ambayo alikuwa akiifanya ya uigizaji wa
filamu za ngono.
Alijua ni lazima kungekuwa na sababu moja kubwa ambayo
ilimfanya Gibson kuamua kufanya uamuzi wa namna ile kwani alijua kwamba Gibson
hakuwa na lengo la kumuacha kwa wakati ule kutokana na sababu kubwa ya kumruhusu
kwa moyo mmoja kuendelea kuigiza filamu za ngono.
Wasiwasi ukaanza kumuingia
Katie kwamba kulikuwa na mtu ambaye alikuwa nyuma ya mpango ule wote,
alichokifanya kwa wakati huo ni kuanza kupeleleza. Kazi ya upelelezi ilikuwa
kubwa sana kitu ambacho kikamfanya kuwaita vijana maalumu kwa ajili ya kuifanya
kazi ile.
Vijana waliifanya kazi ile kwa moyo mmoja, waliangaika kila sehemu
lakini mwisho wa siku hawakupata kitu. Katie akaonekana kuchanganyikiwa,
alichokifanya kwa wakati huo ni kuanza kuyafuatilia maisha ya Gibson
tu.
Alijua fika kwamba Gibson alikuwa akielewa kila kitu juu ya sababu ambazo
zilimfanya kutaka ndoa ivunjwe kwa haraka sana, umuhimu wa kumuuliza Gibson
ulikuwa ukionekana kufaa kwa asilimia zaidi ya mia moja.
Katie akaanza
kugundua vitu fulani, kwanza akaanza kujiuliza juu ya siku ile ambayo Gibson
alikuwa ametekwa na kisha kumwambia kwamba alikuwa amewatoroka watekaji. Swali
ambalo lilikuwa kichwani mwa Katie ni kwa namna gani Gibson alikuwa ameweza
kupigana na watekaji hata bila kujeruhiwa katika sehemu yoyote ya mwili wake na
wakati watekaji wale walikuwa na bunduki?
Katie akaanza kuingiwa na wasiwasi,
akaanza kujua kwamba kulikuwa na kitu ambacho kiliendelea na aliamini kwamba
kitu hicho ndicho ambacho kilimfanya Gibson kutaka kuachana nae na kuuvunja
mkataba wa ndoa ambao walikuwa wameusaini.
“There’s something (Kuna kitu)”
Katie alisema.
Wazo jingine likaingia kichwani mwa Katie, akaanza kugundua
kwamba kulikuwa na kitu ambacho kilikuwa kikiendelea nchini Tanzania ambacho
hicho nacho kilikuwa kimechangia kwa asilimia kubwa kwa Gibson kuamua kufanya
vile.
Katie akaanza kugundua kwamba kulikuwa na uwezekano Gibson alikuwa na
mpenzi nchini Tanzania ambaye alikuwa ameishika akili yake kupita kawaida na
ndio maana alitaka kuachana nae ili aeze kurudi nchini Tanzania na kuendelea na
maisha yake.
Alichokifanya kwa wakati huo ni kuwatuma vijana wake nchini
Tanzania kwa ajili ya kuufanya upelelezi ambao kwake aliuona kumletea majibu
yote. Alihitaji kila kitu kifanyike huku akiwaelekeza kwamba ilikuwa ni lazima
kwao kufikia katika mbuga ya Mikumi ili kupata ukweli juu ya kila kitu kuhusiana
na Gibson.
“Nitawagawia kila kitu, ninachokitaka kutoka kwenu watatu ni
kunipa kila kitu nitakachotaka kukifahamu” Katie aliwaambia vijana wake watatu
ambao walikuwa wakijiandaa kuja nchini Tanzania.
“Sawa! Hautakiwi kuhofia
kitu chochote. Kuna kingine?” Reuben aliuliza.
“Ndio! Kama anaishi na
mwanamke, inatakiwa mmuue kama kisasi changu” Katie aliwaambia.
“Sawa!
Kingine bosi”
“Ni hivyo tu” Katie alisema.
Alichokifanya kwa wakati huo ni
kuwagawia vijana wale kiasi cha dola milioni moja kwa ajili ya kuja nchini
Tanzania huku fedha nyingine akiwatumia pale ambapo wangekuwa wanazihitaji
wakati watakapokuwa nchini Tanzania.
Harakati za kutafuta viza zikaanza
mahali hapo, wala hawakupata tabu kutokana na kuelezea katika ubalozi wa
Tanzania kwamba walikuwa wakitaka kuja nchini Tanzania kwa ajili ya kufanya
utalii tu. Mara baada ya kupata viza, wakakata tiketi za ndege na siku
iliyofuata kuanza safari ya kuja nchini Tanzania kufanya kile ambacho kilikuwa
kikitakiwa kufanyika tu.
****
Reuben, Filbert na Andrew walikuwa ndani ya
ndege ya Gulf Airlines wakielekea nchini Tanzania. Muda wote walikuwa wakiongea
mambo mbalimbali ambayo walitakiwa kuyafanya nchini Tanzania, ramani kubwa ya
nchi ya Tanzania ilikuwa mikononi mwao kwa kuwa walikuwa wakihitaji msaada
mkubwa sana wa kufika kule walipoelekezwa bila kumuuliza mtu yeyote
yule.
Ndege ilichukua masaa zaidi ya ishirini na ndipo ikaanza kutua katika
uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwl Nyerere. Walipofika hapo, hawakutaka kukaa
sana, walichokifanya ni kukata tiketi ya ndege ya kuelekea Morogoro huku lengo
lao likiwa ni kufika katika mbuga ya Mikumi na moja kwa moja kuelekea katika
hoteli iitwayo Mikumi National Park ambako huko ndipo wangeanza kumuulizia mtu
ambaye walikuwa wakimtafuta, Gibson Lyimo.
Safari ya kwenda mkoani Morogoro
ikaanza kwa kutumia ndege ya Precious na baada ya saa moja kuingia mkoani
Morogoro ambako wakaanza kuyafuata magari ya kuelekea katika mbuga hiyo na kisha
kuanza safari. Kila mmoja akilini mwake alikuwa akifikiria lake tu, mtu ambaye
walitakiwa kumuua hakuwa huyo Gibson bali mtu ambaye alitakiwa kuuawa alikuwa
mwanamke ambaye alikuwa akiishi nae katika kipindi hicho.
Walipofika katika
hoteli hiyo iliyokuwa mbugani, wakachukua vyumba na kutulia huku upelelezi
ukifanyika chini kwa chini. Walikaa katika hoteli hiyo kwa muda wa siku mbili na
ndipo walipoamua kumuulizia Gibson kupitia kwa mkurugenzi wa hoteli
hiyo.
“Mnamuuizia Gibson! Huyo mtu aliacha kazi kipindi kirefu cha nyuma. Kwa
sasa hivi ni miongoni mwa watu wenye fedha nyingi sana hapa nchini” Mkurugenzi
wa hoteli hiyo, Massawe aliwaambia.
“Kwa hiyo hatuwezi kupafahamu anapokaa?”
Reuben aliuliza.
“Anakaa Dar es Salaam. Labda kama mnataka kulipia ili
mfanyakazi wangu awapelekea huko mpaka nyumbani kwake” Massawe
aliwaambia.
Reuben na wenzake hawakuwa na jinsi, kitu ambacho walikuwa
wakikitaka kwa wakati huo ni kumfahamu mwanamke ambaye alikuwa akiishi na Gibson
na kisha kufanya kile ambacho walikuwa wameagizwa, walichokifanya ni kumlipa
mkurugenzi na kisha kupewa kijana mmoja ambaye walianza safari nae ya kuelekea
Dar es Salaam.
Njiani hawakukaa kimya, mara kwa mara walikuwa wakimuuliza
maswali mbalimbali kijana yule ambaye walikuwa nae kama namna mojawapo ya
kuchunguza zaidi na kufahamu mambo mbalimbali kuhusiana na jiji la Dar es Salaam
ambalo walikuwa njiani kuelekea uko.
Walipofika Dar es Salaam, moja kwa moja
wakakodi teksi mbili ambazo ziliwapeleka mpaka hotelini na kisha Reuben peke
yake kutoka na kuelekea uko alipokuwa akiishi Gibson huku akiongozana na yule
kijana.
“Do you see that house? (Unaiona nyumba ile?)” Kijana yule
alimuuliza Reuben huku akimuonyeshea nyumba aliyokuwa akiishi
Gibson.
“Please! Stop the car (Tafadhali! Simamisha gari)” Reuben alimwambia
dereva ambaye alisimamisha gari lile.
“Thank you for your help (Asante kwa
msaada wako)” Reuben alimwambia kijana yule huku akimtaka dereva kuwarudisha
hotelini.
“So, why dont you want to meet him? (Kwa hiyo kwa nini hautaki
kuonana nae?)” Kijana yule alimuuliza Reuben.
“I wanted to know the place
(Nilitaka kupafahamu)”Reuben alimwambia.
****
Mchakato bado ulikuwa
ukiendelea kama kawaida, walihitaji kufanya mambo yao kwa haraka haraka hata
kabla wiki haijakatika na kuwakutia ndani ya jiji la Dar es Salaam. Kitu ambacho
walikuwa wakikitaka katika kipindi hicho kilikuwa ni bunduki tu.
Hawakutaka
kumuua mke wa Gibson kwa kutumia silaha yoyote zaidi ya bunduki, wakaanza
kuangalia uwezekano wa kupata bunduki lakini kila walivyoangalia, hawakuona
dalili ya kuweza kuipata aina ya silaha hiyo.
Hawakutaka kujiuliza maswali
mengi sana, wakaona kwamba hata mikono yao ilikuwa na nguvu sana kukabiliana na
huyo mtu tena alikuwa mwanamke, kwao alionekana kutokuwa na usumbufu wowote ule.
Wakajipanga upya, ilikuwa ni lazima utekaji ufanyike, tena kwa haraka
sana.
Hawakujiuliza sana kuhusiana na usafiri ambao wangeutumia siku hiyo,
teksi ya kukodi ndio ambayo ingetumika katika kufanya safari zao za huku na
kule. Walichokifanya mara baada ya kuweka majadiliano ya muda mrefu, wakachukua
ramani ambayo ilikuwa katika begi na kisha kuanza kuiangalia kwa
makini.
Wakaanza kupanga kila kitu kwamba mara baada ya kumaliza kufanya kazi
ambayo ilikuwa imewaleta nchini Tanzania basi ilikuwa ni lazima kuondoka
kuelekea nchini Kenya tena kwa gari kwa kupitia njia ya Tanga, njia ambayo
ingewafanya kutokea Mombasa na kisha huko kupanda ndege na kurudi nchini
Marekani.
Kwao, kazi hiyo wala haikuonekana kuwa ngumu hata kidogo, waliona
kwamba ingeweza kufanyika ndani ya masaa machache hata kabla ya kumtaarifu Katie
na kumwambia kwamba kazi aliyokuwa amewatuma ilikuwa imefanyika, tena kwa
mafanikio makubwa bila kuwa na tatizo hata moja.
Walipanga mambo mengi sana,
walichokuwa wameanza kukifanya ni kuanza kwenda katika mtaa aliokuwa akiishi
Gibson na kisha kuangalia mandhari yote. Hawakuona kama kungekuwa na ugumu sana,
mitaani huko wala hakukuwa na kamera kama ilivyokuwa katika mitaa mingi jijini
New York ambayo ilikuwa ikikaliwa na matajiri, mpaka hapo, tayari wakaiona kazi
hiyo ya kumteka Prisca kuwa nyepesi sana.
Muda mwingi walikuwa wakishinda
ndani ya chumba cha hoteli huku mishemishe yao ikiendelea kama kawaida, kila
kitu ambacho walikuwa wakikipanga kilionekana kutokufaa, hivyo walikifuta na
kuanza kupanga tena.
“I will be a doctor (Nitakuwa daktari)” Reuben
aliwaambia wenzake.
“Ok! We will be your assistants (Sawa! Tutakuwa wasaidizi
wako)” Filbert alimwambia Reuben.
Mpango ambao walikuwa wameufikia kwa wakati
huo ilikuwa ni lazima wajifanye madaktari ambao walikuwa wametoka nchini
Marekani kuja nchini Tanzania kwa ajili ya kuwatibia watoto na kuwapa chanjo
ambayo ingekuwa na uwezo wa kuzuia magonjwa mbalimbali hasa katika kipindi cha
ukuaji.
Wote walikuwa wamekwishajua kwamba Gibson alikuwa akiishi na mwanamke
ambaye alikuwa na mtoto mdogo hivyo kama wangetumia njia hiyo ingekuwa ni rahisi
kwao kumpata mwanamke huyo na kisha kutoroka nae kuelekea porini na kumuulia
huko huko mbele ya safari kabla ya kuanza safari ya kuelea nchini
Marekani.
Mpango ulikuwa umekwishapita, walichokifanya siku hiyo ni kwenda
kwenye kituo kikubwa cha upokeaji na usambazaji madawa, MSD (Medical Store
Departiment) na kisha kuanza kujitambulisha kama madaktari wakubwa ambao
walikuwa wametoka nchini Marekani kwa nia ya kuja hapa kwa ajili ya kuwafanyia
tiba watoto.
Wasimamizi hawakuonekana kufahamu kitu chochote kile, mbaya
zaidi wala hawakuomba hata vitambulisho kutokana na kiasi kikubwa cha fedha
kutolewa kwa kila aliyekuwa na nia ya kuomba vitambulisho vyao hasa katika ngazi
za chini.
Kila mtu ambaye alikuwa akipewa fedha, alikuwa akiwaruhusu kufanya
mambo mengine ambayo wala hayakutakiwa kufanywa kwa mtu yeyote ambaye
hakuonyesha kitambulisho cha kumjulisha kama alikuwa daktari.
“Madawa
hayatoki mpaka nivione vitambulisho vyao” Mkuu wa usambazaji madawa katika
kitengo hicho, mzee Samweli alimwambia msaidizi wake.
“Ila mkuu
inab.....”
“Nimesema hakuna. Kama wao ni madaktari iliwabidi waje na madawa
yao kama watu wengine wanavyofanya. Wanakuja huku halafu dawa wanategemea kwetu,
hauoni kama huu ni ujinga?” Mzee Samweli aliuliza.
“Kama ukiangalia, unaweza
kusema ni ujinga, ila naomba ujifikirie mkuu, ni mara ngapi tumekuwa na vitu
hapa nchini halafu tukashindwa kuvitumia? Wape nafasi waokoe roho za watoto
wetu” Mrisho alimwambia mzee Samweli.
“Sasa wao wameigia ndani ya nchi yao
kama nani? Mbona hatujasikia taarifa za ujio wao?” Mzee Samweli
aliuliza.
“Wamesema kwamba walipokuja hapa hawakuja kama madaktari bali
walikuja kama watalii mkuu” Msaidizi, Mrisho alimwambia Samweli.
“Kumbe ni
watalii! Sasa utalii na udaktari unaingiliana vipi hapo?” Mzee Samweli
aliuliza.
“Wao ni madaktari ambao wamekuja huku kwa ajili ya kufanya utalii
kama sehemu ya mapumziko yao ya likizo. Walipofika hapa, wamesikitishwa na hali
waliyoikuta hasa kwa watoto. Kwa hiyo sasa, wameamua kuuvua utalii na kuuweka
pembeni na kisha kuuvaa udaktari wao na kuingia kazini huku wakiwa na lengo moja
tu, kuwanusuru watoto wetu ambao wapo katika matatizo makubwa hasa katika
kipindi cha ukuaji” Mrisho alielezea kwa kirefu.
“Hebu waite kwanza niwaone”
Mzee Samweli alimwambia Mrisho ambaye aliwaita Reuben na wenzake ndani ya chumba
kile.
Mazungumzo yakaanza upya ndani ya chumba kile. Reuben na wenzake
walikuwa wamevaa nyuso za bandia, nyuso ambazo zilikuwa zikionyesha kwamba
walikuwa na uhitaji wa kuwasaidia watoto wa Kitanzania ambao walikuwa wakikua
huku wakishambuliwa na magonjwa mbalimbali.
Japokuwa walikuwa wakiongea
mengi na kukubalika lakini wakaona kwamba kulikuwa na kitu cha ziada ambacho
kilitakiwa kufanyika zaidi, umwagaji wa fedha ndani ya ofisi hiyo. Hawakutaka
kuchelewa, walianza kujiumauma mwisho wa siku noti za dola mia moja zikawekwa
mezani. Kwa haraka haraka mzee Samweli akazichukua na kuanza kuziangalia,
zilikuwa noti za dola mia moja zilizokuwa kumi.
Kiasi cha dola elfu moja
kilionekana kuwa kiasi kikubwa hasa kwa mtanzania kama mzee Samweli ambaye
maisha yake yalikuwa yakitegemea sana mshahara wa kawaida. Wala hakutaka
kujiuliza kama alitakiwa kuzichukua au kuziacha, alichokifanya ni kuziingiza
mfukoni.
“Mrisho, hebu wapeleke stoo na kisha wape watakachokihitaji” Mzee
Samweli alimwambia Mrisho ambaye alifanya kama alivyoambiwa.
Kwa Mtanzania,
fedha ndio ilikuwa kila kitu, uwepo wa fedha ulikuwa na nafasi kubwa ya
kubadilisha mambo mengi ambayo wala yasingeweza kubadilishwa. Fedha ikaonekana
kuwa kila kitu, fedha hizo hizo ndizo ambazo zilikuwa zikiwafanya Reuben na
wenzake kupelekwa katika stoo ya madawa ambako huko wakachagua madawa
wanayoyataka na kisha kuondoka.
Kazi ilikuwa imebaki moja tu, kwanza ilibidi
kwenda katika serikali ya mtaa wa Masaki na kuelezea kile ambacho kilikuwa
kimewaleta mahali pale, walipofika huko, walimwaga kiasi kidogo cha fedha na
wakaruhusiwa kufanya kazi zao katika mtaa huo.
Hawakuishia hapo, napo
wakaenda mpaka katika hospitali ya Halmashauri iliyokuwepo Masaki na kisha
kuongea na uongozi wa hospitali ambao ulionekana kuwa na furaha kupita kawaida,
Reuben, Filbert na Endrew wakakaribishwa kuanza kufanya kazi katika hospitali
hiyo.
Matangazo yakaanza kufanyika mitaani kwamba kulikuwa na chanjo ambayo
ilikuwa ikitolewa kwa watoto waliokuwa chini ya miaka mitano na hivyo wazazi wao
walitakiwa kuwapeleka watoto wao wao wenyewe kutokana na kutakiwa kuulizwa
maswali mengi kuhusiana na watoto, chanjo hiyo ilitakiwa kufanyika siku
inayofuatia.
“Nitampeleka Genuine huko huko kesho asubuhi” Prisca alimwambia
mumewe, Gibson.
“Ni vizuri sana. Usimwache mfanyakazi ampeleke, si umesikia
kwamba ni mzazi mwenyewe ndiye anayetakiwa kumpeleka?”
“Nimesikia mume wangu.
Nitampeleka tu. Si wamesema mwisho jioni? Nitahakikisha nampeleka hata saa kumi”
Prisca alimwambia Gibson.
“Hapana mpenzi. Nenda uko hata asubuhi. Usikawie,
hauwezi kujua wingi wa watu. Wahi zako asubuhi tu” Gibson alimwambia
Prisca.
“Sawa. Usijali mume wangu” Prisca aliitikia na kulala huku akiwa na
hamu ya kumpeleka mtoto wake akapatiwe chanjo ya kumkinga na magonjwa mbalimbali
katika kipindi chake cha ukuaji.
Je nini kitaendelea?
Je Katie
atakamilisha mpango wake?
IMEDHAMINIWA NA FACEBOOK TAKE AWAY,ZANNEL BONGO LADIES WEAR,MAC AUTO ACCESSORIES,DICK SOUND.
No comments:
Post a Comment