Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa mshtuko na
masikitiko makubwa taarifa ya tukio la leo, Jumapili, Mei 5, 2013 la mlipuko
kwenye Kanisa Katoliki la Mt. Joseph Mfanyakazi la Olasiti Jijini Arusha.
Tukio hilo la kigaidi
limesababisha mtu mmoja kupoteza maisha na wengine 40 kujeruhiwa.
Rais Kikwete analaani vikali shambulio hilo lililofanywa na mtu au watu
katili, waovu na wenye dhamira mbaya na nia mbaya kwa Tanzania na watu
wake.
Rais Kikwete ameagiza
vyombo vya usalama nchini kumsaka mtu au watu waliohusika na kitendo hicho kiovu
na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria. Vile vile Rais Kikwete
amewataka wananchi wote kuwa watulivu wakati Serikali na vyombo vyake inaendelea
kufuatilia tukio hili.
Tutawasaka popote
walipo na kupambana nao bila huruma. Aidha, tutakabiliana na aina
yoyote ya uhalifu nchini iwe ni ugaidi au aina yoyote ya uhalifu wa namna hiyo
au wa namna nyingine, uwe na chimbuko lake ndani ya nchi ama nje ya nchi yetu.
Kamwe hatutakubali
kuwaacha wavuruge amani na usalama wa Tanzania na watu wake. Rais anaamini kuwa
Serikali, kwa msaada na ushirikiano wa wananchi, watu hao watapatikana na
kuadabishwa ipasavyo.
Aidha, Rais Kikwete
anatoa rambirambi za dhati ya moyo wake kwa wafiwa na wale wote ambao
wamejeruhiwa katika tukio hilo. Anaungana nao katika machungu na msiba. Rais pia
anawaombea wote walioumia katika tukio hili wapate nafuu ya haraka na waendelee
na shughuli zao za ujenzi wa taifa.
Rais Kikwete vilevile
anatoa pole nyingi kwa viongozi na waumini wa Kanisa Katoliki kwa tukio hili la
kusikitisha na kuvurugika kwa ibada na shughuli yao muhimu ya uzinduzi wa Kanisa
lao.
Imetolewa
na:
Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais,
IKULU,
DAR ES
SALAAM
5 Mei,
2013
No comments:
Post a Comment