hk CONTACTS

hk CONTACTS

Tuesday, May 28, 2013

MCHEZA FILAMU ZA NGONO SEHEMU YA 13



Mhudumu wa mghahawa wa Casannova ambao ulikuwa katika hoteli ile ile ya Cassanova bado alikuwa akiwahudumia wateja wake, Reuben, Filbert na Andrew kama kawaida yake. Kila wakati alikuwa akiitwa na kurudi huku akiwa na vinywaji mbalimbali mikononi mwake.
Hamadi hakuonekana kuwa na wasiwasi na wateja wale, alikuwa akiendelea kuwahudumia kama kawaida yake. Hakutaka kuongea nao hata kidogo japokuwa moyo wake ulikuwa na shauku kubwa ya kutamani kuongea na wazungu.
Wazungu wale kwake walionekana kuwa tofauti kidogo, walionekana kuwa haraka huku muda mwingi macho yao wakiwa hawayatulizi sehemu moja. Hamadi hakuonekana kujali sana hali ambayo walikuwa nao, kitu ambacho alikuwa akiendelea kukifanya ni kuendelea kuwahudumia kama kawaida tu.
Wateja wote zaidi ya ishirini ambao walikuwa kwenye mghahawa ule walikuwa wamekwishahudumiwa na wakati huo walikuwa wakiendelea kula kitendo ambacho kilimfanya Hamadi na wahudumu wengine wa mghahawa ule kutulia pembeni huku nao wakiangalia televisheni.
Habari ya utekaji ikaanza kutolewa, kila mhudumu alionekana kuwa na utulivu mkubwa kuangalia televisheni ambayo ilikuwa imewekwa kituo cha televisheni ya Taifa. Taarifa ile ikaonekana kumshtua kila mmoja, mtangazaji alikuwa akitangaza kwamba kulikuwa na wazungu watatu ambao walikuwa wamehusika na utekaji wa mwanamke mmoja na mtoto mmoja ambaye alikuwa na umri wa takribani mwaka mmoja.
“Watekaji hao wanakisiwa kukimbilia mkoani Kilimanjaro, Tanga, Arusha au Manyara” Mtangazaji alisema huku akionekana kutokuwa na uhakika.
Hapo ndipo ambapo Hamadi alipoanza kuwaangalia wazungu wale ambao walikuwa mezani. Kwanza akaanza kuwahesabu kwamba walikuwa watatu kama ambavyo mtangazaji alikuwa ametangaza kwenye televisheni, akawaangalia tena, wawili nywele zao zilikuwa nyeupe na mmoja nywele zake zikuwa nyeusi, nao wale wazungu walikuwa vile vile.
Kila kitu ambacho kilikuwa kikitangazwa kuhusiana na watekaji nyara wale, kilikuwa kikifanana sana na wazungu wale ambao walikuwa wamekaa katika mghahawa ule. Hamadi akashindwa kuvumilia, tayari alikuwa na uhakika kwamba wale watekaji ambao walikuwa wakizungumziwa kwenye televisheni walikuwa wale wazungu ambao walikuwa katika mghahawa ule.
Alichokifanya Hamadi ni kutoka na kuanza kuelekea jikoni. Alipofika huko, akachomoa simu yake na kuanza kupiga namba za polisi ambazo zilikuwa zikijulikana sana 911. Simu ikaanza kuita, wala haikuita muda mrefu, ikapokelewa na sauti nzito ya mwanaume kusikika.
“Karibu katika kitengo cha usalama wa Taifa” Sauti ile ilisikika.
“Hallow. Naitwa Hamadi hapa, nipo Tanga Mjini barabara ya kumi na tatu” Hamadi alisema huku akionekana kuwa na haraka.
“Kuna tukio lolote lile limetokea huko?”
“Ndio. Hapa kwenye mghahawa nawaona watu watatu ambao taarifa zinasema kwamba wanatafutwa na jeshi la polisi kwa tukio walilolifanya la utekaji” Hamadi alisema.
“Sawasawa. Wapo vipi hao watu?”
“Ni wazungu watatu. Wana kila sifa ambazo mtangazaji wa televisheni alivyotangaza” Hamadi alisema.
“Upo Tanga sehemu gani?”
“Barabara ya kumi na tatu katika hoteli ya Cassanova hapa. Fanyeni haraka, naona kama wanataka kuondoka” Hamadi alisema na kisha kukata simu.
Hamadi akarudi tena ndani ya mghahawa. Reuben na wenzake bado walikuwa wakiendelea kunywa kama kawaida yao, walichukua dakika mbili tu baada ya Hamadi kutoka jikoni wakasimama, wakalipia na kuondoka mahali hapo.
Hamadi aliwaona polisi wakichelewa kufika mahali hapo, alionekana kuwa na shauku ya kuwaona polisi wakifika hapo, wakiwakamata na kisha kupewa zawadi nono ambayo ilikuwa imeandaliwa kwa mtu yeyote ambaye angefanikisha kukamatwa kwa watu wale.
Wala hazikupita dakika nyingi, defender ya polisi ikasimama nje ya mghahawa ule na kisha polisi kuruka chini kikomandoo na kuelekea ndani ya mghahawa ule ambapo moja kwa moja wakamhitaji Hamadi.
“Wapo wapi?” Polisi mmoja alimuuliza huku akiwa ameshika bunduki.
“Wameondoka muda mchache uliopita”
“Unajua wameelekea wapi?”
“Wameelekea kule upande wa kaskazini”
“Wamekwenda na gari gani?”
“Starlet nyeusi”
“Sawa. Twende garini tuwafuate” Polisi yule alisema.
Hamadi hakuwa na wasiwasi, alichokifanya ni kupanda ndani ya defender ile ambayo ilikuwa na polisi zaidi ya kumi ambao walikuwa na bunduki na kisha kuanza kuelekea kule gari lile la watekaji lilipoelekea.
Mpaka kufikia kipindi hicho polisi wakawa na uhakika kwamba watekaji wale walikuwa njiani kuelekea mpakani mwa nchi ya Tanzania na Kenya, kuingilia ndani yamji wa Mombasa. Dereva wa defender lile alikuwa akiendesha kwa mwendo wa kasi sana, mpaka kufika ndani ya dakika ishirini, walikuwa wakiliona gari lile kwa mbele umbali wa nusu kilometa.
“Watakuwa ndio wenyewe wale. Ongeza kasi dereva” Polisi ambaye alionekana kuwa kiongozi alimwambia dereva.
Gari likaongezwa kasi, kila polisi ambaye alikuwa na bunduki akaanza kuikoki bunduki yake. Tayari muda wa vita ukaonekana kufikia, walitakiwa kupambana kiume mpaka kuona kwamba wanawaokoa mateka ambao walikuwa wameshikiliwa.
Gari lile la watekaji likaenda kwa umbali fulani, wakaliona likikata kona upande wa kushoto na kuingia porini, nao walipofikia eneo lile, wakakata kona na kuingia porini. Tayari mpaka kufikia kipindi hicho walikuwa na uhakika kwamba watu wale walikuwa watekaji na kulikuwa na uhakika wa asilimia mia moja kwamba mateka wale bado walikuwa nao.
Wakaendelea kuelekea kule porini mpaka kufika sehemu ambayo kulikuwa na gari lile tu. Walipoanza kulisogelea na kulifikia, hakukuwa na mtu yeyote yule zaidi ya khanga moja tu ambayo alikuwa ameivaa Prisca. 
Wakaanza kusogea mbele zaidi mpaka kufika sehemu ambayo wakaanza kusikika minong’ono ya watu. Wakajificha na kuanza kuchungulia kule minong’ono ilipokuwa ikitokea, macho yao yakatua kwa watekaji wale huku Reuben akiwa amemkaba Prisca ambaye alikuwa akijitahidi kujitoa katika roba ile.
Kila mmoja alijua kwamba ule ndio ulikuwa mwisho wa Prisca, polisi mmoja ambaye alikuwa akisifika kwa shabaha akaandaa bunduki yake tayari kwa kuwalenga. Mapolisi walionekana kutokuwa na wasiwasi hata kidogo, tayari walikwishagundua kwamba watekaji wale wala hawakuwa na bunduki yoyote ile.
“Mlenge yule aliyemkaba mwanamke yule” Polisi kiongozi alimwambia.
“Kichwani au wapi?”
“Usimuue. Mlenge kwenye ule mkono uliomkaba mwanamke”
“Nimekuelewa”
Mlio wa risasi ukasikika mahali hapo, Reuben akaanza kupiga uyowe mkubwa sana, damu zilikuwa zikimtoka mkononi ambao ulikuwa umepigwa na risasi. Filbert na Andrew wakaona kwamba tayari kila kitu kilikuwa kimeharibika, walichokifanya ni kuanza kukimbia.
Polisi yule wa shabaha wala hakuwa na haraka, alichokifanya ni kuilenga miguu yao, wote wakajikuta wakianguka chini kama mizigo huku wakilia kama watoto. Hawakutaka kumuacha Reuben vile vile, nae akapigwa risasi nyingine ya mguu, hawakutaka mtu yeyote yule atoroke kutoka katika mikono yao.
“Kweli una shabaha” 
“Hii ndio kazi yangu bwana. Hata ungeniambia nilenge jicho, ningelilenga tu”
Polisi wale wakawasogelea na kisha kuwachukua. Wote walikuwa wakilia kwa maumivu makali, risasi zile zilikuwa zimepenya miguuni mwao. Baadhi ya polisi wakaanza kumsogelea Prisca, walipogusa mapigo yake ya moyo, alikuwa akihema kwa mbali sana.
“Tuondokeni” Kiongozi alisema na kisha wote kuingia ndani ya gari huku mapolisi watatu wakiingia ndani ya ile Starlet pamoja na Prisca ambaye alikuwa kimya na safari kuelekea Tanga mjini kuanza.
****
Manase alikuwa akiendesha gari kwa mwendo wa kasi huku Gibson akiwa pembeni yake. Mawazo ya Gibson kwa wakati huo hayakuweza kutulia hata kidogo, muda wote alikuwa akiiwaza familia yake, mke wake, Prisca pamoja na mtoto wake, Genuine.
Akili yake wala haikutulia hata kidogo, kama kuhuzunika tayari alikuwa amehuzunika sana kiasi ambacho wakati mwingine alikuwa akishikwa na hasira hata zaidi ya simba aliyejeruhiwa. Maswali kibao yalikuwa yakijazana kichwani kwake kuhusiana na watekaji ambao alikuwa na uhakika kwamba walikuwa wametumwa na msichana Katie, msichana ambaye alikuwa amemuoa na kuachana nae kwa sababu kulikuwa na mtu mwingine ambaye alikuwa akimhitaji zaidi.
Hakukuwa na mtu ambaye alikuwa akiongea kitu chochote ndani ya gari, kila mtu alikuwa kimya huku wakionekana kuifuatilia kwa ukaribu safari hiyo ambayo kwao waliiona kwamba ingezaa matunda kwa kile kitu ambacho walikuwa wakikifuata.
“Wanasemaje? Wamewakamata?” Gibson alimuuliza Manase ambaye alikuwa amemaliza kuongea na simu.
“Bado wanaendelea na upekuzi wa kila gari. Nadhani tunaweza kukutana nao njiani pia” Manase alimjibu Gibson.
Safari bado ilikuwa ikiendelea kama kawaida tena gari likiendeshwa kwa mwendo wa kasi sana. Baada ya umbali fulani, wakafika katika eneo ambalo lilikuwa na watu kadhaa wasiozidi ishirini ambao walikuwa wamezunguka kitu karibu na kichaka huku mikono yao ikiwa kichwani.
Hawakutaka kusimama wala kushuhudia ni kitu gani ambacho kilikuwa kikiendelea mahali pale, walichokifanya ni kuendelea na safari yao huku wakionekana kuwa na haraka kupita kawaida bila kujua kwamba watu walewalikuwa wameizunguka maiti ya genuine ambaye alikuwa ametupwa wakati gari likiwa katika mwendo wa kasi. Safari iliendelea zaidi na zaidi mpaka kufika Segera, hakukuwa na mtekaji yeyote ambaye alikuwa amekamatwa na polisi wale.
Kila mmoja alionekana kuchanganyikiwa, hawakuonekana kuelewa mahali ambapo watekaji wale walikuwa wamepitia. Kila mmoja alionekana kutokuelewa, mpaka kufikia muda huo hawakuwa na uhakika kama watekaji wale walikuwa wamekwishavuka mahali hapo au bado.
Kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo walionekana kuchanganyikiwa zaidi, kwanza hawakutaka kuendelea na safari yao, walichokifanya ni kupaki gari pembeni hapo Segera na kuanza kuongea kuona nini kilitakiwa kufuata.
“Kwa hiyo tufanye nini?” Dokta Phillip aliuliza.
“Bado sijajua. Yaani hapa nimekwishachanganyikiwa kabisa. Sijui hawa watekaji watakuwa wamepita njia gani na wakati watu kule Chalinze waliwaona wakichukua njia hii” Manase alisema huku akiitoa simu yake.
Muda wote huo Gibson alikuwa amebaki kimya, kichwa chake kilikuwa kikiifikiria familia yake tu. Hakujua mahali ambapo watekaji wale walipokuwa wameichukua familia yake. Muda wote moyo wake ulikuwa ukifahamu kwamba ni msichana Katie ndiye ambaye alikuwa ameucheza mchezo mzima mpaka kufikia muda huo.
“Huku hawajafika” Manase aliongea simuni.
“Hawajafika? Hawajafika vipi na wakati watu wamekamatwa Tanga?” Sauti ya pili ilisikika.
“Wamekamatwa Tanga?” Manase aliuliza huku akionekana kushtuka.
Swali lile likamfanya Gibson pamoja na dokta Phillip kumsogelea Manase ambaye bado alikuwa akiongea na simu kutoka makao makuu ya kituo cha polisi kilichokuwa jijini Dar es Salaam. Aliongea kwa sekunde kadhaa na kisha kukata simu.
“Wamekamatwa mkoani Tanga” Manase aliwaambia huku akionekana kutabasamu.
“Asante Yesu! Na vipi kuhusu familia yangu?” Gibson aliuliza.
“Hilo sijauliza. Cha msingi twendeni Tanga” Manase aliwaambia.
Hakukuwa na kitu kingine cha zaidi cha kufanya zaidi ya kuingia ndani ya gari na safari ya kuelekea Tanga kuanza mara moja. Muda mwingi Gibson alikuwa akiuliza swali lakini maswali yake hayakuwa na majibu zaidi ya kutakiwa kusubiria mpaka pale ambapo wangeingia Tanga na kuangalia kama familia yake ilikuwa salama.
Safari iliendelea kwa muda wa dakika arobaini na tano, wakawa wamekwishafika Tanga ambako wakaelekea mpaka katika kituo kikubwa cha polisi cha mkoa huo. Kutokana na kujulikana na mapolisi wenzake, Manase akaingia mpaka ndani.
“Wapo wapi?” Manase alimuuliza polisi mmoja.
“Wapo ndani”
“Mateka nao wamepatikana?”
“Kwani walikuwa wangapi?”
“Wawili” Manase alijibu.
“Ndio. Ila sisi tumefanikiwa kumpata mmoja tu”
“Yupi?”
“Mwanamke”
“Mliangalia vizuri garini na kuona kwamba hakukuwa na mtoto?”
“Ndio. Tena gari lao lenyewe tumekuja nalo. Nadhani tukiwabana watatueleza mtoto yupo wapi” Polisi huyo alimwambia Manase.
“Kwa hiyo huyo mwanamke yupo wapi?”
“Hospitalini. Kijana mmoja alikuwa akitaka kumuua kwa kumnyonga shingo. Bahati nzuri shabaha za Shabani zilitusaidia” Polisi yule alijibu.
“Mmempeleka hospitali gani?”
“Hospitali ya mkoa”
“Hali yake ilikuwaje?”
“Mbaya. Yaani mbaya sana”
Manase hakutaka kuendelea kukaa ndani ya chumba kile, alichokifanya kwa wakati huo ni kutoka nje na kisha kumfuata Gibson ambaye akaanza kumuelezea kile ambacho alikuwa ameelezewa na polisi aliyekuwa ndani ya chumba kile.
Gibson alionekana kuchanganyikiwa zaidi, hasira kali dhidi ya watekaji wae ikaonekana kumkaba, walichokifanya kwa wakati huo ni kuingia ndani ya gari na kisha kuanza kuelekea hospitalini ambako wala hapakuwa mbali kutoka mahali hapo.
Ndani ya gari bado Gibson alionekana kuwa na hasira kupita kawaida, chuki juu ya Katie ikaanza kumuingia moyoni mwake na kuzidi kuongezeka kadri muda ulivyozidi kwenda mbele. Alimchukia sana Katie, kwake, tayari aliona kwamba kila kitu kilikuwa kimekwisha, hakuona sababu iiyompelekea Katie kuamua kuwatuma watu kuja nchini Tanzania kwa ajili ya kuiteka familia yake.
“Nitamuua huyu mwanamke” Gibson aliwaambia huku akionekana kuwa na hasira za waziwazi.
“Achana nae. Kwanza tuangalie hali ya mke wako” Manase alimwambia Gibson.
“Sawa! Ila haijalishi kama atapona au atakufa. Nitamuua tu” Gibson alimwambia.
“Nakushauri uiachie sheria ili ichukue mkondo wake. Unaweza kujuta hapo baadae kwa kujichukulia sheria mkononi” Manase alimwambia Gibson ambaye alionekana kutokuelewa kabisa.
Baada ya dakika chache wakawa wamekwishafika katika hospitali ya mkoa wa Tanga na kisha kuteremka. Moja kwa moja wakaanza kupiga hatua kuelekea sehemu ya mapokezi ambako wakajitambulisha na kisha kuelekezwa sehemu ambayo walitakiwa kuelekea.
“Twendeni kwa dokta mkuu kwanza” Manase aliwaambia.
“Kwa nini tusielekee kwenye chumba alicholazwa mke wangu na mtoto wangu?” Gibson aliuliza bila kujua kwamba mtoto wake hakuwepo mahali hapo
“Muda wa kuona wagonjwa umekwishapita na ndio maana nawaambia twendeni huko ili tuongee nae na kuturuhusu” Manase aliwaambia.
Hakukuwa na mtu yeyote ambaye alionekana kupinga, walichokifanya ni kuanza kuelekea katika ofisi ya dokta mkuu na kukaribishwa. Uso wa Gibson haukuonekana kuwa na furaha kabisa, muda wote alikuwa akionekana kuwa na majonzi makubwa.
Wakaanza kujitambulisha kwa dokta Mnyuzu na kisha kutaka kupatiwa maelezo yanayotosheleza kuhusiana na mgonjwa wao ambaye alikuwa ameletwa ndani ya hospitali ile ya mkoa. Hata kabla ya kuongea kitu chochote kile, dokta Mnyuzu akakaa kimya kwa muda huku akiwaangali kwa zamu, aliporidhika, akayagandisha macho yake usoni mwa Gibson.
“Mwanamke yule ni mke wako?” Dokta Mnyuzu alimuuliza Gibson.
“Ndio” Gibson alijibu.
“Pole sana. Ni habari mbaya lakini haina budi kukupa. Wewe ni mwanaume, nakuomba ujikaze kiume” Dokta Mnyuzu alimwambia Gibson ambaye hapo hapo akaonekana kuishiwa nguvu, akakiegemeza kichwa chake huku akimwangalia Dokta Mnyuzu.
“Mkeo amefariki” Ilikuwa ni sauti ambayo ilikuwa ikisikika mara kwa mara kichwani mwa Gibson.

Je nini kitaendelea?
Je Prisca amekufa?
Je Gibson atafanya nini akisikia hali ya mkewe?

Tusisahau uzinduzi wa video ya majanga jumapili @new maisha club dar.snura atasindikizwa na madee,mirror,ali nipishe,timbulo,baucha na wema sepetu ndio atakaeizindua video ya majanga.
uzinduzi huu umedhaminiwa na DICK SOUND,HUSEIN PAMBA KALI,1 TED,CLOUDS FM,CELAGEM na XTREME DEEJAYZ.usikose.

No comments:

Post a Comment