hk CONTACTS

hk CONTACTS

Monday, June 3, 2013

MCHEZA FILAMU ZA NGONO SEHEMU YA MWISHO 15



  MCHEZA FILAMU ZA NGONO 15

Watanzania bado walikuwa wakiendelea kulaani kitendo kile cha utekaji ambacho kilikuwa kimefanyika. Muda mwingi watu walikuwa wakitembea na mabango kuelekea katika ubalozi wa Marekani. Maandamano yalikuwa yamefanyika kwa takribani siku tatu mfululizo jambo lililompelekea balozi wa Marekani nchini Tanzania kuwasiliana na serikali ya Marekani ili kuanza kufuatilia kuhusu vijana wao, ikiwezekana harakati zote zifanyike mpaka hukumu ya watekaji wale kufanyika.
Waandishi wengi wa habari walikuwa wakifika katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kuanza kuongea na Gibson ambaye muda mwingi alikuwa akionekana kuwa mnyonge kupita kawaida. Mtu ambaye alikuwa akisubiriwa apate fahamu ni Prisca tu ambaye angeeleza kila kitu na hata mahali ambapo mtoto Genuine alikuwa ametupwa.
Siku zikaendelea kukatika, wazazi wote wa pande mbili pamoja na ndugu na marafiki wa karibu walikuwa wakifika hospitalini pale kwa ajili ya kumjulia hali Prisca ambaye mpaka wiki imekatika lakini bado hakuwa amerudiwa na fahamu. 
“Kipindi kirefu kimepita. Hii inaonekana kuwa si kawaida kabisa” Gibson alimwambia dokta Marwa ambaye alikuwa akimshughulikia Prisca kila siku.
“Mshipa wake wa fahamu umeshtuka sana. Mara nyingi watu ambao wanapatwa na tatizo hili huwa wanatumia muda mrefu kitandani. Mshipa wa fahamu unaposhtuka kwa nguvu, huwa wakati mwingine unaweza kuufanya hata uti wa mgongo kupata matatizo. Na ikitokea uti wa mgongo kupata tatizo, mgonjwa anaweza akapooza sehemu moja ya mwili” Dokta Marwa alimwambia Gibson maneno ambayo yalionekana kumshtua.
“Kwa hiyo mke wangu atapooza?” 
“Sikuwa na maana hiyo. Hapo nimejaribu kukwambia kitu ambacho mara nyingi hutokea. Mkeo anaweza kurudiwa na fahamu na wala asipate tatizo lolote lile” Dokta Marwa alimwambia Gibson.
Yalikuwa ni maneno makali ambayo yaliuumiza sana moyo wa Gibson, muda mwingi alikuwa akionekana kuwa na wasiwasi kupita kawaida, meneno yale ambayo aliambiwa kwamba mke wake angeweza kupooza yalikuwa yamemtiwa wasiwasi kupita kawaida. Upweke ukaongezeka maishani mwake, kwa wakati huo wala hakutaka kusimamia biashara zake ambazo zilikuwa zikiendelea kumuingizia mamilioni, muda mwingi alikuwa akiutumia kuwa karibu na kitanda alicholazwa mke wake.
“Utarudi katika fahamu zako mpenzi na kuniambia mtoto wangu walimtupa sehemu gani. Hata kama atakuwa amekufa, nitahitaji kuliona hata kaburi lake tu” Gibson alikuwa akimwambia mkewe ambaye bado alikuwa kwenye usingizi wa kifo.
Maisha ya kutokwa na machozi yakawa sehemu ya maisha yake, kila siku alikuwa mtu wa kulia sana jambo ambalo lilikuwa likimpelekea kudhoofika mwili wake kupita kawaida. Watu mbalimbali walikuwa wakimtembelea na kumfariji lakini wala hawakuweza kubadilisha kitu chochote kile, kila siku Gibson alikuwa mtu wa kulia tu.
Wiki ya pili ikakatika, wiki ya tatu ikaingia lakini hakukuwa na mabadiliko yoyote yale. Bado Prisca alikuwa kwenye usingizi wa kifo jambo ambalo lilionekana kuwachanganya hata madaktari wenyewe. Mirija ambayo ilikuwa ikipitishwa katika sehemu yake ya tumbo ndio ambayo ilikuwa ikitumika kumlisha chakula pamoja na kumywesha maji.
“Au amekwishakufa?” Gibson alimuuliza dokta Marwa.
“Hapana. Bado ni mzima. Hata moyo wake unadunda. Tuvumilie hadi mshipa wa fahamu utakapokuwa sawa” Dokta Marwa alimwambia Gibson.
Hakukuwa na cha kufanya kwa wakati huo, waliendelea kusubiri zaidi na zaidi. Mwezi ukakatika, hakukuwa na mabadiliko yoyote ya maendeleo, bado Prisca alikuwa amelala kitandani huku moyo wake ukidunda kwa mbali sana.
****
Katie alikuwa akijiandaa kutoka mtoko wa usiku pamoja na Daniel ambaye alipanga waonane katika mghahawa wa Mc Donald kwa ajili ya kupata chakula cha usiku pamoja na kununua Ice Cream ambazo zilikuwa zikipendwa sana. Huo ulikuwa ni mtoko ambao ulikuwa ukiwahusisha watu wawili ambao walikuwa wameishi sana katika maisha ya mitaani kipindi cha nyuma na wakati huo walikuwa matajiri wakubwa.
Kila vazi ambalo alikuwa akilivaa Katie lilionekana kutokumpendeza jambo ambalo lilimfanya kubadilisha kila aina ya vazi ambalo alikuwa ameliweka katika kabati lake kubwa la nguo. Alianza na gauni jekundu ambalo lilikuwa na maua mawili kiunoni, hilo hakuliona kumfaa kwa siku hiyo, akaamua kuliweka pembeni.
Hapo ndipo alipoamua kuchukua gauni jingine ambalo lilikuwa na rangi mbalimbali zilizopangwa kimpangilio huku likiwa na vitu vilivyokuwa vikinga’aa sana, hilo nalo akaliona kutokufaa kwa usiku huo. Mtoko huo kwake ulionekana kuwa mtoko mmoja mkubwa sana ambao ungewafanya kuongea mambo mengi, kupeana mapenzi na Daniel na hata kufanya mapenzi kama siku ile ya kwanza ambayo walifanya.
Alibadilishabadilisha mavazi zaidi ya kumi na mbili usiku huo na ndipo alipolipata vazi moja ambalo kwake lilionekana kuwa zuri katika usiku huo wa siku hiyo. Baada ya kumaliza kujiandaa, akajipulizia manukato mazuri ambayo yalikuwa na gharama na kisha kulifuata gari lake na kuanza kuelekea katika mghahawa huo.
Ndani ya gari, mawazo yake kwa kipindi hicho yalikuwa yaimfikiria Daniel tu, Gibson kwa wakati huo wala hakutaka kumpa sana nafasi kichwani mwake. Aliona kwamba kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea kati yake na Gibson kilitakiwa kusahaulika katika maisha yake na kujipanga upya na Daniel.
Kwa wakati mwingine alikuwa akiwafikiria vijana wake ambao alikuwa amewatuma kwa kufanya kazi moja ya kumuua mwanamke ambaye alikuwa akiishi na Gibson kwa wakati huo. Mpaka kufikia kipindi hicho wala hakuwa amepata taarifa zozote kutoka kwa vijana wake tangu siku mbili zilizopita ambazo zilikuwa siku za mwisho kuongea nao.
Wala Katie hakuchukua muda mrefu akawa amekwishafika katika mghahawa huo ambao mara nyingi sana ulikuwa ukitembelewa na masupastaa nyakati za usiku na kisha kuanza kupiga hatua kuelekea katika meza ambayo Daniel alikuwepo. Mara tu Daniel alipomuona Katie, akainuka na kuanza kumsogelea, alipomfikia, akamkumbatia na kumshushia mabusu kadhaa ya mdomoni.
Wakaifuata meza na kukaa huku mhudumu akija na wote kuagiza chakula ambacho walikiona kufaa sana kula siku hiyo. Wakabaki wakiongea mengi, katika kipindi hicho ndio ulikuwa muda muafaka wa kukumbushiana mambo mengi ya nyuma yaliyopita, hasa katika kipindi kile ambacho walikuwa watoto wa mitaani.
Kipindi kile kilionekana kuwa kipindi kizuri kwao wote, walikula na kinywa huku wote wakionekana kuwa na furaha. Furaha ambazo walikuwa nazo katika kipindi hicho ndizo ambazo ziliwafanya kupeana ahadi ya kuishi pamoja kama mume na mke mara kila kitu kitakapokaa sawa. 
Baada ya hapo, moja kwa moja wakaanza safari ya kuelekea katika hoteli ya Pasiphian ambayo ilikuwa kando ya jiji hilo la New York na kisha kulala huko. Usiku wa siku hiyo kwao ukaonekana kuwa usiku wa kukumbuka, walipeana mapenzi ya dhati mpaka kufikia kipindi ambacho kila mtu alikuwa hoi kitandani.
Asubuhi ya siku iliyofuata, wakaongozana wote na kuelekea nyumbani kwa Katie. Hali ambayo waliikuta nyumbani hapo ilionekana kumshtua kila mmoja. Nje, kulikuwa na magari mawili ya polisi huku mapolisi wawili wakiwa nje ya eneo la nyumba ile na huku wengine wakiwa wamekwishaingia ndani ya eneo la nyumba ile.
Katie akaonekana kushtuka, akateremka kutoka garini na moja kwa moja kuwafuata mapolisi ambao walikuwa nje ya nyumba yake. Kitu cha kwanza walichokifanya mapolisi wale mara baada ya kumuona ni kuanza kumsogelea.
“What the hell is going on here? (Kitu gani kinaendelea mahali hapa?)” Katie aliuliza huku akionekana kushangaa.
“We are looking for you mom (Tunakutafuta wewe)” Polisi mmoja alimwambia.
Hapo hapo mapolisi wale wakamwambia dhumuni la wao kufika mahali pale na kisha kumwambia kupanda ndani ya gari huku wale mapolisi ambao walikuwa ndani ya eneo la nyumba yake wakiwa wamekwishafika mahali pale.
Daniel ambaye alikuwa amekwishateremka garini akaanza kuwafuata na kisha kuanza kuwauliza maswali kadhaa ambayo hakukuwa na polisi yeyote ambaye aliyajibu maswali yale. Moja kwa moja safari ya kuelekea katika kituo kikuu cha polisi katika jiji hilo la New York kuanza huku tayari Katie akionekana kuanza kuhisi kitu.
Walipofika kituoni, akateremshwa na kisha kuanza kupelekwa ndani ya jengo hilo ambako akaingizwa ndani ya chumba kimoja kwa ajili ya kuulizwa maswali kadhaa. Polisi mmoja ambaye alivalia suti akaingia ndani ya chumba kile na kisha kuanza kumuuliza maswali kadhaa huku akimtolea picha ambazo walipigwa Reuben, Filbert na Edward nchini Tanzania jambo ambalo lilimfanya kuona kwamba hisia zake zilikuwa zimehusika moja kwa moja na kile ambacho alikuwa akikihisi.
“I want to talk to my lawyer (Nataka kuongea na Mwanasheria wangu)” Katie alimwambia polisi yule kila alipoona maswali yakizidi kuulizwa.
Huo ndio ulikuwa mwanzo wa kesi hiyo ulipoanza huku Reuben na wenzake wakiwa wamepelekwa nchini Marekani. Kwa kuwa Prisca bado alikuwa amepoteza fahamu, Gibson na dokta Philip ndio ambao walikuwa mashahidi wa kwanza katika kesi hiyo ambayo ilikuwa ikivuma sana katika vyombo mbalimbali vya habari duniani.
Kesi ilivuma zaidi ya miezi mitatu, Katie akakutwa na hatia ambayo ikampelekea kufungwa miaka ishirini jela huku vijana wake ambao alikuwa amewatuma kufanya mauaji wakifungwa miaka ishirini na tano jela.
Hiyo ilionekana kuwa hukumu kubwa kwa Katie, muda wote mahakamani alikuwa akilia huku akijaribu kumuomba msamaha Gibson ambaye alishindwa kuvumilia na machozi kumtoka. Hilo halikuweza kubadilisha kitu chochote kile, siku hiyo ndio ambayo Katie alikwenda kuanza kukitumikia kifungo chake katika gereza la South Greeen, gereza lililokuwa kusini mwa jiji la New York nchini Marekani.
Japokuwa Katie alikuwa amefungwa lakini Daniel hakutaka kuachana nae, bado mapenzi ambayo alikuwa nayo kwa Katie yalikuwa makubwa. Mara kwa mara alikuwa akimtembelea gerezani na baada ya mwaka mmoja kufunga ndoa pamoja katika kanisa la gereza lililokuwa hapo hapo gerezani.
Japokuwa maisha yalionekana kuwa magumu, lakini katika kipindi ambacho alikuwa akionana na mke wake Katie yalikuwa yakionekana kuwa rahisi sana. Furaha ikaonekana kutawala katika mahusiano yao japokuwa walikuwa wakiishi tofauti sana. Kwa kuwa walikuwa mume na mke, kila walipokuwa wakikutana walikuwa wakipewa uhuru wa kufanya kila kitu mpaka pale Katie alipojifungua mtoto wa kiume na kumuita jina la Hope kwa kutumaini kwamba kuna siku angetoka gerezani na kuishi pamoja na familia hiyo.
“I love you Katie.....I love you Katie (nakupenda Katie....Nakupenda Katie)” Daniel alimwambia Katie muda mchache mara baada ya kujifungua huku wakiwa wamekumbatiana na mtoto Hope akiwa mikononi mwa Katie.
“I love you too (Nakupenda pia)” Katie alimwambia Daniel.
****
Miezi sita ilikuwa imekatika lakini Prisca hakuweza kurudiwa na fahamu zake. Kila siku Gibson alikuwa akiomba Mungu lakini sala zake zilionekana kutokujibiwa kabisa. Hali ya mke wake, Katie ilikuwa ikimuumiza kila siku, kila alipokuwa akimuona pale kitandani alikuwa akiumia kupita kawaida.
Moyo wake bado ulikuwa na mapenzi ya dhati kwa mke wake huyo ambaye kwake alionekana kuwa kama mfu kitandani pale. Kila siku marafiki zake pamoja na ndugu zake walikuwa wakifika hospitalini pale kwa ajili ya kumuona Prisca ambaye alikuwa hajafumbua macho yake.
Siku ziliendelea kukatika mpaka pale Gibson alipokwenda nchini Marekani kusimamia kesi ya mauaji ambayo ilikuwa ikiwakabiri watu wanne. Kwa jinsi alivyokwenda na kurudi baada ya miezi mitatu wala hakukuwa na mabadiliko yoyote yale, Prisca hakuwa amefumbua macho yake, alikuwa kama jinsi alivyomuacha kabla ya kuondoka.
Siku ziliendelea kukatika. Ilipofika tare 5 mwezi wa 7, siku hiyo ilionekana kuwa kama muujiza kwa Prisca, kwa mara ya kwanza baada ya miezi mingi, akaweza kufumbua macho yake tena. Tukio lile likaonekana kumshtua kila mtu, manesi wote waliona jambo lile kuwa kama muujiza ambao wala hawakuwa wakiutegemea. Kitu walichokifanya ni kumpigia simu dokta Marwa ambaye akafika mahali hapo na kushuhudi kwa macho yake. PRISCA ALIKUWA AMERUDIWA NA FAHAMU.
****
Dokta Marwa hakuweza kuvumilia, kitu alichokifanya kwa wakati huo ni kuchukua simu yake na kisha kumpigia Gibson ambaye baada ya dakika thelathini akawa amekwishafika ndani ya eneo la hospitali hiyo na moja kwa moja kuelekea katika chumba kile. Gibson hakuweza kuyaamini macho yake, machozi ya furaha yakaanza kumtoka, akaanza kumfuata Prisca pale kitandani na kisha kumkumbatia. Muda wote Prisca alikuwa akimshangaa Gibson, kwake alikuwa akionekana kuwa kama mtu mpya. 
“Umeamka. Umeamka hatimae” Gibson alimwambia Prisca ambaye bado alikuwa akimshangaa.
Kwa haraka sana Gibson akaichukua simu yake na kisha kuwapigia wazazi wake na kisha kuanza kuwaambia kuhusu muujiza ambao ulikuwa umetokea hospitalini. Wazazi wa pande zote mbili wakafika mahali hapo. Mara Prisca alipowaona wazazi wake, tabasamu pana likatawala uso wake.
Huo ndio ulionekana kuwa muujiza mkubwa. Prisca hakuwa na nguvu za kuongea japokuwa alikuwa amefumbua macho. Baada ya mwezi mmoja kupita, Prisca akaruhusiwa kurudi nyumbani huku kila kitu ambacho alikuwa akikiona kilionekana kuwa kipya machoni mwake.
“Nimewakumbuka sana. Mdogo wangu Dorice yupo wapi?” Prisca aliuliza huku akionekana kuwa mwenye furaha.
“Amekwenda chuoni” Mama yake, Bi Magreth alijibu.
“Mnanitania. Lini ameanza chuo? Si yupo kidato cha pili?” Prisca aliuliza swali ambalo lilimshangaza kila mtu.
“Unasemaje?”
“Toka lini mwanafunzi wa kidato cha pili akaanza chuo?” Prisca aliuliza.
Kila mmoja alionekana kushtuka, si wazazi tu ambao walionekana kushtuka bali hata Gibson mwenyewe alikuwa ameshtuka kupita kawaida. Hakujua ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea, kila wakati alikuwa akijiuliza kama tukio la kupoteza kumbukumbu lilianza kumfanya kuwa chizi au la.
“Prisca! Unamjua huyu?” Baba yake, mzee Steven alimuuliza huku akimnyooshea Gibson kidole.
“Hapana” Prisca alijibu.
“Haumjui?”
“Ndio. Ni mgeni amekuja leo au?” Prisca aliuliza swali ambalo lilionekana kumshtua kila mtu.
“Ila sisi unatujua?”
“Ndio. Ninyi ni wazazi wangu”
“Ila huyu haumjui?”
“Simjui kabisa. Sidhani kama nilikwishawahi kumuona mtu huyu. Mara ya kwanza kumuona ilikuwa pale hospitalini, nilishangaa kumuona akinikumbatia. Siku nyingine alikuwa akiniletea zawadi pale hospitalini. Kitu cha ajabu, ninyi hamkuonekana kujali, yaani mimi kutembelewa na kuletewa zawadi na mtu nisiyemfahamu mlikuwa mkiona kuwa ni jambo la kawaida sana na wakati nilikuwa nikifikiria sana” Prisca aliwaambia wazazi wake.
“Ok! Kuna mtu yeyote unamkumbuka?” Mzee Steven alimuuliza.
“Namkumbuka rafiki yangu, Pamela, Happy, Everlyn. Hivi Vonso amekwisharudi kutoka Uganda?” Prisca aliuliza maswali ambayo yaliendelea kumshangaza kila mtu.
Hiyo ndio hali ambayo ilikuwa imemtokea Prisca. Mshipa wake wa kumbukumbu ulikuwa umeharibika sana, katika kipindi hicho alikuwa akiwakumbuka watu ambao alikuwa akiishi nao katika kipindi ambacho alikuwa kidato cha tatu. Hakumkumbuka tena mume wake Gibson, kila alipokuwa akimwangalia, kwake alionekana kuwa mtu mgeni.
Prisca hakukumbuka kitu chochote kile, alikuwa akiwakumbuka wazazi wake pamoja na marafiki zake kwa sababu tu alikuwa ameishi nao katika kipindi kirefu. Hakukumbuka kama alikuwa ameolewa, hakukumbuka kama alikuwa amezaa mtoto ambaye alikuwa ameuawa zaidi ya kujishangaa kila alipokuwa akiyaminya matiti yake na kuona yakitoa maziwa.
“Nini kimenitokea mama?” Prisca alimuuliza mama yake.
“Kuna nini?”
“Matiti yangu. Nashangaa yanatoa maziwa kama mwanamke aliyejifungua” Prisca alimwambia mama yake.
“Mmmh! Hebu kesho twende hospitalini, linaweza kuwa tatizo la kiafya” Mama yake alimjibu.
Hayo ndio maisha yake yalivyokuwa. Prisca huyu alikuwa tofauti na Prisca yule ambaye alikuwa akikumbuka kila kitu. Hapo ndipo ambapo Gibson alipoanza kazi ya kuuteka moyo wa Prisca kwa mara nyingine tena. Mara kwa mara alikuwa akienda nyumbani kwao ambako huko alikuwa akikaa nae sana na kuongea pamoja.
Kila walipokuwa wakiongea, Gibson alikuwa akijisikia uchungu moyoni, hakuamini kama mke wake alikuwa amemsahau. Kazi ya kuuteka moyo wa Prisca kwa mara nyingine haikuwa rahisi ingawa alikuwa akijitahidi kadri ya uwezo wake. Mara kwa mara alikuwa akitoka nae na kuelekea ufukweni, katika mighahawa mbalimbali ili mladi kumfanya Prisca kuangukia katika mapenzi yake kwa mara nyingine.
“Unaonekana kama unaniogopa Prisca” Gibson alimwambia Prisca.
“Hapana Gibson. Unajua nahitaji muda zaidi wa kukuzoea. Unaponiona hivi, usijali. Tutaendelea kuzoeana tu” Prisca alimwambia Gibson.
Gibson hakutaka kukata tamaa, kila siku alikuwa akiangaika kumfanya Prisca amzoee na hatimae atamke neno ‘Nakupenda’ mbele ya macho yake. Hali hiyo iliendelea zaidi na zaidi, ukaribu wao ukaendelea kadri siku zilivyozidi kwenda mbele. Mwezi wa kwanza ukapita, mwezi wa pili ukaingia huku bado Gibson akiendelea kumfanya Prisca kujisikia kuwa huru nae.
“Lini utamwambia kwamba unampenda?” Mzee Steven alimuuliza Gibson.
“Muda bado. Ukifika, nitamwambia. Akikubali, nitamuoa kwa mara ya pili tena na kuzaa nae mtoto mwingine” Gibson alimjibu mzee Steven
Hiyo ndio hali ilivyokuwa, kila siku Gibson alikuwa akijitahidi kumfanya Prisca amzoee zaidi na zaidi. Kwa sababu yeye ndiye alikuwa amesababisha hayo yote basi hakuwa na budi kuangaika kumfanya Prisca ampende kwa mara ya pili hasa mara baada ya kupoteza kumbukumbu yake ya miaka saba iliyopita.
“Nitaendelea hivi hivi mpaka nitakapokuja kumuoa kwa mara nyingine tena” Gibson alikuwa akijisemea katika kipindi ambacho alikuwa akielekea Zanzibar pamoja na Prisca kwa ajili ya kuangalia mambo mbalimbali yaliyoachwa na wakoloni.
MWISHO 


TOKA UANZE KUSOMA, ULIIPENDA SANA HADITHI HII NA HUJAWAHI KUJITAMBULISHA KWANGU KWAMBA NAWE U MFUATILIAJI. HEBU KWA LEO PIGA LIKE YAKO MOJA, SEMA CHOCHOTE THEN MAISHA YAENDELEEE. ILA KAMA HAUJAIPENDA, IPOTEZEE.

SHUKRANI KWA WADHAMINI WANGU 
zannel bongo ladies wear,mac auto assecories,dick sound,husein pamba kali,masa celagem,xtreme deeejayz.na wote mliokuwa mnaifatilia hadithi hii. soon naanza na IGIZO JIPYA LA KAHABA TOKA CHINA.asante wote na mzee wa harakati za bongo.

2 comments:

  1. kaka umetsha xana nmependa simuliz yako ina visa vinavyotoa hamu ya kuendelea kuisoma...ila nahic inaweza kufanyiw movie

    ReplyDelete
  2. Dah! Hadithi tamu hadi najisahau kama nasoma hadithi, nahisi kama ishu imetokea kweli vile! Mkubwa wewe ni MKALI!

    ReplyDelete