Tayari mambo
yalikwishaanza kuwa magumu kwa Gibso
n, simu ambayo alikuwa ameipokea kutoka
kwa Daniel ikaanza kumtia kiwewe kupita kawaida. Hakutulia, muda wote alikuwa
amkimsisitizia Katie kwamba ilikuwa ni lazima wauvunje mkataba wa ndoa yao ili
aweze kuikoa nafsi yake ambayo ilikuwa ikisakwa sana.
Baada ya kulalamika
sana, Katie akakubali kishingo upande. Moyoni mwake ilikuwa imemuuma kupita
kawaida, mapenzi yake makubwa bado yalikuwa kwa Gibson ambaye kwa wakati huo
alitaka wavuje mkataba wa ndoa wa miaka mitano ambao walikuwa
wameandikishiana.
Walichokifanya ni kuelekea mahakamani ambako huko mkataba
ukavunjwa. Ingawa Gibson alikuwa akifanya hivyo lakini moyo wake ulikuwa
ukimuuma kupita kawaida. Nguvu ya fedha ndio ambayo ilikuwa imempelekea kufanya
kitu kama kile ambacho wala hakuwa akitaka kukifanya.
“Nitarudi Tanzania tu.
Tena haraka iwezekanavyo” Gibson alijisemea.
Alikaa nchini Marekani kwa siku
mbili zaidi huku akionana na Daniel ambaye alikuwa akimpa pongezi kwa kile
ambacho alikuwa amekifanya, na baada ya hapo, akakata tiketi na kurudi nchini
Tanzania kwa kutumia ndege ya American Airlines.
Ndani ya ndege hakuwa na
raha hata kidogo, kwanza akili yake ilikuwa ikimfikiria sana Katie ambaye
alikuwa amemuacha katika hali ya unyonge mkubwa huku akiwa amemuumiza kupita
kawaida. Ukiachilia na Katie, pia mawazo yake yalikuwa yakimfikiria mke wake
aliyemuacha nchini Tanzania, Prisca pamoja na mtoto wake, Genuine.
Gibson
hakujua kama Prisca alikuwa amekwishajua kilichoendelea au la. Kitu ambacho
alikuwa akitaka kukifanya mahali hapo ni kuusoma mchezo tu. Kwanza angeangalia
Prisca angempa mapokezi gani, hapo ndipo ambapo angegundua kwamba siri ilikuwa
imevuja au bado iliendelea kuwa siri.
Alitumia zaidi ya masaa ishirini katika
ndege ile na ndipo ndege ilipotua katika uwanja wa Mwl Julius Nyerere huku ikiwa
ni saa tisa usiku. Kwa sababu ilikuwa ni usiku sana, Gibson hakutaka kurudi
nyumbani, alichokifanya ni kwenda kulala kwenye hoteli ya New African.
Usiku
wala hakulala, kichwa chake kilikuwa kikiwafikiria watu wawili kwa wakati huo.
Kwa Katie, alijiona kufanya uamuzi mkubwa na mgumu kufanyika, kuna wakati
mwingine alijiona bora amefanya uamuzi ule kwani ulikuwa na manufaa kuliko
kuendelea kuishi na mwanake huyo ambaye alikuwa akicheza filamu za
ngono.
Katika kichwa chake, kwa wakati mwingine alikuwa akimfikiria sana mke
wake, Prisca. Hakujua mwanake huyo angesema kitu gani hasa mara baada ya kuishi
nchini Marekani kwa zaidi ya miezi sita bila kuwasiliana nae. Akili yake ikaanza
kufikiria uongo mbalimbali ambao alitakiwa kumwambia Prisca mara baada ya kufika
nyumbani kwake.
“Nitamdanganya tu, wanawake ni rahisi sana kuukubali uongo”
Gibson alijisemea.
“Mmmh! Lakini miezi sita bila mawasiliano! Hivi kama
isingekuwa Daniel si mpaka mwaka ungetimia bila kufanya mawasiliano na Prisca.
Kweli nilifanya kitu kibaya sana” Gibson alijisemea na kisha kupatwa na usingizi
huku ikiwa imetimia saa kumi na mbili alfajiri.
Alikuja kuamka ikiwa saa saba
mchana muda ambao aliagiza chakula na kuletewa chumbani na kisha kuanza kula.
Kichwa chake kwa wakati huo kilikuwa kikifikiria namna ya kumwambia Prisca ili
aweze kumuelewa. Ni kweli kwamba alitunga uongo mbalimbali lakini kwa wakati ho,
kila uongo ambao alikuwa ameutunga ulionekana kutokufaa, yaani aliuona kuwa
uongo wa kitoto.
Ilipofika saa tisa, akajitoa mhanga na kuanza kuelekea
nyumbani kwake. Kadri gari ilivyokuwa ikizidi kusogea na ndivyo ambavyo wasiwasi
ulivyokuwa ukimshika zaidi na kuufanya moyo wake kududa kupita
kawaida.
Alichukua dakika thelathini hadi kufika nyumbani ambako akateremka
ndani ya taksi na kisha kumlipa dereva na kuanza kulifuata geti la nyumba yake.
Mapigo yake ya moyo yakazidi kudunda zaidi na zaidi kana kwamba kulikuwa na
hatari kubwa mbele yake. Alipolifikia geti, akabonyeza kengele na mlinzi kuja
kufungua.
“Karibu sana kaka” Mlinzi alimkaribisha huku akimpokea
begi.
“Subiri kwanza. Shemeji yako yupo?” Gibson aliuliza hata kabla
hajaingia ndani.
“Hayupo. Aliondoka kwenda kwa wazazi wake” Mlinzi
alimjibu.
“Dah! Toka lini?”
“Mwezi wa tano huu” Mlinzi alimjibu Gibson
jibu ambalo likaonekana kumtia wasiwasi.
“Duh! Kwa nini sasa?”
“Nilimsikia
Rehema akisema kwamba kisa kilikuwa picha”
“Picha gani?”
“Hakutaka
kuniambia”
“Ok! Rehema mwenyewe yupo?”
“Ndio” Mlinzi alijibu.
Gibson
akaanza kupiga hatua kuingia ndani na kisha kuufuata mlango wa kuingilia
sebuleni. Kwa wakati huo alikuwa akitaka kuongea na Rehema ambaye alikuwa
mfanyakazi wa ndani na kisha kumuuliza kuhusu picha ambazo mpaka hapo
zikaonekana kumchanganya.
“Picha gani?” Gibson alimuuliza Rehema.
“Kuna
picha alipewa zikionyesha kwamba ulipiga na mzungu” Rehema alijibu.
“Sasa
kupiga picha na wazungu si kawaida sana hasa unapokuwa Marekani au Ulaya. Kipi
hasa kilichomfanya kuondoka hapa nyumbani?” Gibson aliendelea kuuliza.
“Hizo
hizo picha”
“Picha?”
“Ndio. Ulipiga ukiwa na mwanamke wa kizungu ambaye
alikuwa amevaa shela la harusi huku wewe ukiwa umevaa suti, yaani lilionekana
kuwa tukio la kufunga ndoa” Rehema alimwambia Gibson ambaye akabaki
kimya.
Tayari kila kitu kiichoendelea nchini Marekani kikaonekana kujulikana
kwa Prisca, kwa maana hiyo kama Prisca aliweza kuujua ukweli basi iliwezekana
hata wakwe zake na wazazi wake walikuwa wakiufahamu ukweli. Kitu alichokifanya
mahali hapo ni kutoka nje, kuchukua gari na kisha kuanza kuelekea nyumbani kwao
huku akioneknana kuchanganyikiwa.
Tayari kwa wakati huo alijiona kufanya
makosa makubwa, asingeweza kuelekea nyumbani kwa kina Prisca bila wazazi wake,
alichokuwa akikifanya kwa wakati huo ni kumfuata baba yake, mzee Lyimo pamoja na
mama yake ili waweze kuelekea nyumbani kwa kina Prisca kwa ajili ya kumuombea
msamaha kwa kila kilichotokea nchini Marekani.
“Umefanya upumbavu mkubwa
sana” Mzee Lyimo alimwambia Gibson kwa sauti ya juu.
“Nafahamu baba, nafahamu
kwamba nimefanya kosa kubwa lakini ninahitaji kusamehewa pia kama ambavyo
ninaomba msamaha” Gibson alimambia baba yake.
“Yaani umetutia doa hata sisi
wenyewe. Tumeonekana tumekulea katika maisha ya ajabu ajabu. Eti unaondoka hapa
na kuelekea Marekani kufunga ndoa, tena na mwanamke malaya ambaye anacheza
filamu za ngono. Huo ni ujinga sana” Mzee Lyimo alisema maneno ambayo yalimfanya
Gibson kushtuka.
Hapo ndipo alipogundua kwamba wazazi wake walikuwa
wakifahamu kila kitu kilichoendelea na hadi kazi ambayo Katie alikuwa akiifanya
ilikuwa imekwishagundulika. Kwake, tayari mambo yakaanza kuonekana kuwa magumu,
alijua fika kwamba kwa hatua ile ambayo alikuwa amefikia, ilikuwa ngumu sana kwa
Prisca kuweza kumsamehe.
Gibson akaanza kueleza kila kitu ambacho kilikuwa
kimetokea katika maisha yake pamoja na Katie, wazazi wake walikuwa kimya huku
wakimsikiliza kwa makini kwani walihitaji kufahamu kila kitu kuona ni kwa namna
gani wangeweza kuwaelezea wazazi wenzao ili kukubaliana nao na kumsamehe
Gibson.
“Kwa hiyo ukaamua kuvunja mkataba wa ndoa?” Mzee Lyimo
alimuuliza.
“Ndio. Niliamua kuuvunja kwa sababu nilijiona kuwa na uhitaji
mkubwa wa kuja Tanzania na kumuona mke wangu na mtoto wangu. Kamwe nisingeweza
kukaa zaidi bila kuwaona wao” Gibson alidanganya.
Gibson, mzee Lyimo na mama
yake, Bi Yustina wakaanza kuelekea nyumbani kwa mzee Steven huku lengo lao
likiwa ni kumuombea msamaha kijana wao ambaye alikuwa ameamua kutubu dhambi zake
juu ya kile ambacho alikuwa amekifanya nchini Marekani.
Walipofika nyumbani
kwa mzee Steven, wote wakateremka na kuanza kuelekea getini kisha mlinzi
kuwafungulia na kuanza kuingia ndani ya eneo la nyumba hiyo. Wakaanza kuufuata
mlango wa kuingilia sebuleni ambao wakaugonga na kukaribishwa ndani.
Mzee
Steven na mkewe, Bi Magreth walikuwa sebuleni hapo, walipowaona wazee wenzao
wanaingia, wakawakaribisha kwa furaha lakini mara walipomuona Gibson akiingia
pamoja nao, wakabadilika kabisa. Nyuso za furaha ambazo walikuwa nazo zikawa
zimekwishabadilika kabisa, walionekana dhahiri kutokumpenda Gibson kwa wakati
huo. Hata pale Gibson alipowasalimia, hakukuwa na mtu aliyeitikia.
Wakakaa
kochini na kisha kuanza kuongea na baadae kumpa ruhusa Gibson kuongea. Ila kabla
hajaanza kuongea, Prisca akaitwa mahali hapo, alipomuona mume wake, akaanza
kulia. Prisca alikuwa mgumu kubembelezeka, alizidi kulia zaidi na zaidi huku
Gibson akiangalia chini kwa aibu.
Prisca alilia kwa muda mrefu, aliponyamaza,
Gibson akaanza kuelezea kila kitu ambacho kilitokea katika maisha yake na Katie
tangu kipindi kile walipokutana kazini. Gibson alikuwa mkweli, ila katika sehemu
moja tu hakutaka kuwa mkweli, hakutaka kuwaeleza wazazi wake kwamba alikuwa
amevunja mkataba wa ndoa kwa sababu alipewa kiasi kikubwa cha fedha,
alichokisema yeye ni kwamba alivunja mkataba wa ndoa kwa sababu alijua kile
alichokuwa akikifanya kutokuwa kizuri, hivyo alihitaji kurudi nyumbani kuishi na
mkewe aliyekuwa akimpenda.
Alipomaliza kuelezea kila kitu akaanza kuomba
msamaha. Ilikuwa ni ngumu sana kwa Prisca kumsamehe Gibson kwa sababu kile
alichokuwa amemfanyia kilikuwa kitu kibaya sana kilichomuumiza moyo wake.
Yalipita masaa mawili huku Gibson akiomba msamaha huku akilia kama mtoto na
ndipo Prisca akaamua kumsamehe tena huku msaada wa wazazi wao ukiwa umesaidia
kwa asilimia kubwa.
Baada ya hapo, Gibson akaamua kuishi na mke wake, Prisca
kwa amani, hakutaka kusikia kitu chochote kutoka kwa mwanamke Katie. Moyoni
mwake hakujua kabisa, hakujua kwamba alikuwa amemjeruhi sana Katie, na hivyo
muda si mrefu kuanzia hapo angetaka kulipiza kiasi kwa kile kilichotokea. Huko
Marekani, Katie alikuwa amebadilika, alikuwa kama mbogo aliyejeruhiwa huku
akimtafuta mtu aliyemjeruhi.
Baada ya hapo, maisha yataanza kubadilika,
huzuni itaingia, hasira za Katie zikabadilisha kila kitu, furaha ikawa huzuni na
majonzi. Kwa Gibson hilo wala hakulitambua, alikuwa akiendelea kuishi na Prisca
huku akijua kwamba yeye na Katie yalikuwa yamekwisha, kumbe ilikuwa tofauti
kabisa kwani ndio kwanza mambo yalikuwa yakianza tena ngoma ikiwa mbichi
kabisa...na kama gazeti, ndio kwanza ulikuwa umeanza ukurasa wa
kwanza.
Je nini kitaendelea?
Je Katie atafanya nini kudhirisha hasira
zake?
Je maisha yataendelea kuwa ya furaha kwa Gibson na mkewe,
Prisca?
Itaendelea kesho saa nne usiku.
imedhaminiwa na dick sound mnyama,mac auto accessories,zannel bongo ladies wear na f
acebook take away watengenezaji wa chips tamu kinondoni.
No comments:
Post a Comment