Pages

Monday, May 20, 2013

MCHEZA FILAMU ZA NGONO SEHEMU YA 8



Katie alikuwa chooni huku akiwa amefungwa kamba mikononi mwake na kisha ile kamba kufungwa katika bomba. Muda mwingi alikuwa akipiga kelele za kuomba msaada lakini wala hakukuwa na mtu yeyote ambaye alifika mahali hapo na kumsaidia.
Katie hakutaka kukata tamaa, aliendelea kupiga kele zaidi na zaidi. Kichwa chake kwa wakati huo kilikuwa kikimfikiria mume wake ambaye alikuwa ametekwa na kupelekwa asipopafahamu. Alitamani kuifungua kamba ile na kisha kuichukua simu ambayo ilikuwa mfukoni mwake lakini kitu kile kilionekana kuwa kigumu kufanyika.
Tayari mambo yakaonekana kuwa magumu kwa upande wake, kamwe asingeweza kuendelea kupiga kelele kama asingeonyesha jitihada za kutaka kujisaidia yeye mwenyewe. Alichokifanya mahali hapo ni kuanza kuzifungua kamba zile kwa kutumia meno yake.
Japokuwa mara ya kwanza kazi ilionekana kuwa rahisi sana lakini baadae ikaonekana kuwa ngumu tofauti na hisia zake. Alijitahidi kufungua zaidi na zaidi, alichukua zaidi ya dakika thelathini na ndipo ambapo kamba zile zikafunguka.
Akaanza kuugonga mlango wa choo kile, aligonga zaidi mpaka pale ambapo muuzaji wa mafuta alipokuja na kisha kuufungua mlango wa choo kile. Nywele za Katie zilikuwa zimevurugika sana, zilikuwa timtim kama chizi. Akaanza kuelezea kile kilichokuwa kimetokea na kisha kupiga simu polisi.
Kila mwananchi ambaye aligundua kwamba mwanamke yule aliyekuwa amesimama mbele yao alikuwa Katie, wengi wakatamani kutaka kupiga nae picha, uadimu wa kukutana na masupastaa waliokuwa wakiishi nchini mwao ndio ilikuwa sababu mojawapo iliyomfanya kila mmoja kutaka kupiga picha na Katie japokuwa alikuwa katika hali mbaya.
Ndani ya dakika tano, polisi wakaingia mahali hapo na kisha kuanza kuchukua maelezo ya awali ya Katie na kisha kumpakiza garini na kuondoka nae. Garini, Katie hakuwa na amani, alikuwa akimfikiria mume wake ambaye alikuwa ametekwa na watu ambao wala hakuwa akiwafahamu.
Maswali mfululizo yalikuwa yakijikusanya kichwani mwake juu ya watekaji wale ambao walikuwa wamemteka mume wake mpendwa. Hakujua kama mpaka katika kipindi hicho Gibson alikuwa mzima au alikuwa ameuawa. Amani haikupatikana moyoni mwake, muda wote alikuwa akitokwa na machozi tu.
Alipofikishwa katika kituo kikuu cha polisi cha New York, akaanza kutoa maelezo kwa kirefu zaidi. Katika kila kitu ambacho alikuwa akikieleza mahali hapo, polisi mmoja alikuwa akiandika katika faili lake ambalo lilikuwa mezani. Kila kitu kilipokamilika, akaruhusiwa kuelekea nyumbani huku mapolisi wakianza kazi yao.
Katie akarudi mpaka nyumbani, moyo wake ulikuwa katika maumivu makali kupita kawaida. Hisia kwamba Gibson alikuwa ameuawa zikaanza kumjia kichwani kitu ambacho kikamfanya kuwa na wasiwasi kupita kawaida. Muda mwingi alikuwa akilia tu, miezi sita ambayo alikuwa amekaa na mume wake ulionekana kuwa muda mfupi sana, alikuwa akihitaji kuwa nae zaidi na zaidi mpaka pale ambapo mkataba wa ndoa yao ungeisha na kufikiria ni kitu gani ambacho kingeendelea maishani mwao.
Katie hakutaka kubaki kimya, akaanza kuwataarifu marafiki zake na ndugu zake na kisha kuwaelezea kile ambacho kilikuwa kimetokea jambo ambalo liliwafanya wafike nyumbani hapo kwa ajili ya kumfariji. Hakujua ni nani ambaye aliwapata taarifa waandishi wa habari, lakini ndani ya nusu saa tayari walikuwa wamekwishafika nyumbani hapo na kisha kuanza mahojiano nae.
Katie hakutaka kuficha, akaanza kuelezea kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea bila kuficha kitu hata kimoja. Kila mmoja akaonekana kushangaa, utekaji wa mtu mkubwa haukuwa umefanyika kwa kipindi kirefu sana nchini Marekani, utekaji ambao ulikuwa ukifanywa mara nyingi ulikuwa ni wa watoto tu.
Lengo la watekaji wala halikueleweka kabisa, waandishi wa habari, polisi pamoja na watu wengine ambao walikuwa wamesikia kila kiichotokea wakaonekana kushangaa kupita kawaida. Tayari kukaonekana kuna namna, tena kitu ambacho walikuwa wamekifikiria zaidi ni kwamba watekaji hao walikuwa wamekwenda kumuua Gibson.
‘Hata kama watamuua....nitataka kuuona mwili wake” Katie alisema huku akilia kama mtoto na ndugu, marafiki zake wakimfariji.
******
Milio mitatu ya risasi ilikuwa imesikika mahali hapo, uso wa Daniel ulikuwa ukionyesha tabasamu pana kama njia mojawapo ya kuonyesha kwamba tayari alikuwa amekamilisha kile ambacho alikuwa ametaka kifanyike mahali hapo.
Gibson alibaki kimya huku akitetemeka, hakuamini kama risasi zile tatu ambazo zilikuwa zimepigwa, zilikuwa zimepita pembeni yake. Haja ndogo tayari ilikuwa imekwishamtoka, alikuwa akitetemeka kwa hofu kubwa. Japokuwa alikuwa na miaka zaidi ya ishirini lakini hiyo ndio ilikuwa mara yake ya kwanza kuusikia mlio wa risasi.
Gibson akaanza kujipapasa kuona kama kweli hakukuwa na risasi ambayo ilikuwa imepenya mwilini mwake, mwili wake ulikuwa vile vile, wala haukuwa umejeruhiwa kwa risasi yoyote ile jambo ambalo lilimfanya kumwangalia Daniel ambaye uso wake ulikuwa ukionyesha tabasamu pana.
“Kama nikitaka kukuua, naweza kukuua sasa hivi, tena ndani ya sekunde moja tu. Ila ukiona risasi imepita pembeni yako, basi jua sitaki kukuua” Daniel alimwambia Gibson ambaye alikuwa kimya huku akizidi kutetemeka.
Daniel hakutaka kuendelea kumnyooshea bunduki Gibson kitu ambacho kilimfanya kuiweka kiunoni mwake na kisha kuanza kumsogelea. Tayari Daniel alikwishaona kwamba kama angeendelea kuishika bunduki ile basi kusingekuwa na maelewano yoyote yale ambayo yangeweza kufanyika mahali hapo, aliona kuwa na uhitaji wote wa kuweza kuificha bunduki ile kutoka mbele ya Gibson ili waweze kuongea vizuri na kufikia muafaka.
“Nimekuacha kwa sababu moja kubwa” Daniel alimwambia Gibson ambaye bado alikuwa akionekana kuwa na wasiwasi na kuendelea.
“Kitu kikubwa ambacho ninakitaka kutoka kwako, achana na Katie. Yule ni msichana wangu ninayempenda sana kutoka moyoni. Ninapoongea sasa hivi, nataka uachane nae” Daniel alimwambia Gibson.
“Itakuwa ngumu sana” Gibson alimwambia Daniel.
“Kwa nini?”
“Mkataba wa ndoa yetu haujakwisha kabisa. Ndio kwanza miezi sita imekatika” Gibson alimwamba Daniel.
“Hata kama. Ninachotaka uachane nae tu. Nitakupa ofa kama utaweza kufanya hivyo ndani ya wiki moja” Daniel alimwambia Gibson.
“Ofa gani?”
Hilo ndilo swali ambalo Daniel alikuwa akitaka kulisikia kutoka kwa Gibson. Alijua fika kwamba Gibson alikuwa akimpenda sana Katie ila aliona kuwa kama alitaka watu hao watengane basi ilikuwa ni lazima afanye kitu kimoja kikubwa, atumie fedha tu.
Kumfuata Katie na kumrubuni kwa fedha ili aachane na Gibson lilikuwa jambo gumu sana na hii ilikuwa kwa sababu msichana huyo alikuwa na kiasi kikubwa cha fedha. Gibson, kwake ndiye ambaye alionekana kuwa mtu mzuri ambaye angeweza kuyazima mapenzi aliyokuwa nayo kwa Katie kama tu angeweza kumuahidi kiasi fulani cha fedha.
“Nina dola milioni kumi. Nataka uachane na Katie tu” Daniel alimwambia Gibson.
Gibson akajiona kama kutokusikia vizuri kile ambacho alikuwa ameambiwa, alimwangalia Daniel mara mbili mbili huku akionekana kutokuamini kile ambacho alikuwa ameambiwa mahali pale. Akaileta kalkuleta ya kichwani mwake, akazibadilisha fedha zile katika thamani ya fedha za kitanzania, zilikuwa zaidi ya bilioni ishirini, yaani angepata zaidi ya shilingi bilioni ishirini tu endapo angefanikisha kuachana na Katie.
Ofa ile ikaonekana kuwa nzuri kwake, hakuamini kama mwisho wa siku angeweza kupata kiasi kikubwa namna ile kwa kufanya kitu kidogo tu, cha kuachana na Katie. Tamaa ya fedha ambazyo alikuwa nayo ikazidi kuota mizizi moyoni mwake, alikuwa radhi kumfanyia Katie kitu chochote isipokuwa kumuua endapo tu angeahidiwa kiasi cha fedha kama kile ambacho alikuwa ameahidiwa.
Hakutaka kujiona chizi, hakutaka kujiona kutokuwa na bahati, ofa ile ilikuwa ni vigumu sana kukatalika moyoni mwake, na si kwa yeye tu bali hata kwa Watanzania wote ambao walikuwa wakikaa nchini Tanzania. Kumuacha Katie kwake wala hakukuonekana kuwa na tatizo lolote lile.
“Ofa imekubalika” Gibson alimwambia Daniel maneno ambayo yalimfanya Daniel kutabasamu zaidi.
“Ila inakubidi kuwa makini” Daniel alimwambia Gibson.
“Umakini gani?”
“Nitazituma fedha katika akaunti yako, nataka ndani ya wiki, kila kitu kiwe kimefanikiwa, usipofanikisha ndani ya wiki. Nitakuua. Umesikia?” Daniel alimwambia Gibson.
“Ndio”
“Ok! Kumbuka ni ndani ya wiki tu” Daniel alisisitiza.
“Sawa”
Daniel akaonekana kuwa mwenye furaha zaidi, alionekana kufurahia sana kwa kuwa Gibson wala hakuonekana kuwa mgumu kuikubali ofa ile. Alichokifanya mahali hapo ni kutoa karatasi na kumkabidhi Gibson na kisha kuandika akaunti yake ya benki ambayo angependa fedha hizo ziingizwe.
“Mbona namba hii ngeni machoni mwangu?” Daniel aliuliza mara baada ya kuiona namba ambayo Gibson alikuwa ameiandika.
“Hiyo ni namba ya akaunti yangu ya nchini Tanzania. Nataka nikiachana nae tu nirudi nchini Tanzania. Au wazo baya hilo?” Gibson aliuliza.
“Wazo zuri. Tena zuri sana” Daniel alimwambia Gibson na kisha kumruhusu kuondoka mahali hapo kuelekea garini tayari kwa kurudi jijini New York pamoja nao.
Muda wote Gibson alikuwa akionekana kuwa na furaha kupita kawaida, kila siku maisha yake alikuwa akiyaona kuwa na bahati kubwa. Alikumbuka kwamba alikuwa amesoma katika shule za kawaida sana na wala hakufikiria kama angekua tajiri, lakini kwa sababu ya mapenzi tu, yakamfanya kuwa tajiri nchini Tanzania.
Huku akiendelea kuumiliki utajiri mkubwa, kiasi kikubwa cha fedha ambazo angeweza kukiingiza kwa miaka mitatu, alikuwa akikiingiza ndani ya masaa machache tu, yaani pale ambapo angemwambia Katie kwamba ule ndio ulikuwa mwisho wa mahusiano yao, kwa maana hiyo wangeachana na kurudi nchini Tanzania.
Walipita katika njia nyingine kabisa mpaka kutokea jijini New York ambako wakamuacha. Gibson akaanza kutembea kuelekea katika stesheni ya treni na kisha kupanda treni na kuelekea nyumbani kwake, pembeni mwa jiji hilo la New York. Kichwa chake kwa wakati huo kilikuwa kikifikiria kitu kimoja tu, kufika nyumbani na kumwambia Katie kwamba asingeweza kuendelea nae tena na hivyo mkataba wa ndoa yao uvunjwe haraka iwezekanavyo.
“Mmmh! Nitaanzia wapi sasa hadi kumwambia tuvunje ndoa?” Gibson alijiuliza.
“Ila poa. Nitajua nimwambie nini” Alijijibu mwenyewe.
*****
Gibson akaingia ndani, waandishi wa habari ambao walikuwa ndani ya eneo la nyumba hiyo kwa ajili ya kumhoji Katie wakaanza kumsogelea huku wakiviweka mbele vyombo vyao vya kuekodia sauti. Kila mwandishi akaonekana kumshangaa Gibson, wakati huo habari ilikuwa ikiripotiwa kwamba alikuwa ametekwa, je kwa nini alikuwa mahali hapo muda huo? Je aliwatoroka watekaji au walimuacha? Na kama walimuacha bila kumjeruhi, lengo lao la kumteka lilikuwa nini?
Kila mwandishi ambaye alikuwa akijiuliza maswali hayo hakupata jibu, mtu pekee ambaye angewapa majibu ya kutosha na kuridhisha alikuwa mmoja tu, Gibson. Gibson hakutaka kuongea kitu chochote kile, alichokifanya ni kuendelea kupiga hatua mpaka ndani ya nyumba yake.
Katie, ndugu zake na marafiki zake wa karibu wakashtuka, hawakuamini kama Gibson alikuwa akiingia ndani ya nyumba ile kwa wakati ule na wakati alikuwa ametekwa masaa kadhaa yaliyopita. Katie akashindwa kuvumilia, akainuka, akaanza kupiga hatua kumfuata Gibson, alipomfikia, akamkumbatia kwa furaha.
Katie akashindwa kuyazuia machozi yake ya furaha, yakaanza kumtoka huku akiwa bado amemkumbatia Gibson. Gibson akaanza kumbembeleza Katie kwamba kwa wakati huo hakutakiwa kuhofia kitu chochote kile kwa sababu alikuwa amerudi akiwa mzima wa afya kama alivyokuwa ametekwa.
Katie akamjitoa mwilini mwa Gibson na kisha kuanza kumwangalia kwa mtindo wa kumchunguza. Alikuwa akimwangalia kwa makini kama alikuwa amejeruhiwa au la. Mwili wake ulikuwa vile vile, hakukuwa na jeraha lolote lile.
“What happened to you? (Nini kilikutokea?)” Katie alimuuliza Gibson.
“I ascaped (Nilitoroka)” Gibson alijibu.
“Thank you Jesus! I was just worring about you. Where did they take you to? (Asante Yesu! Nilikuwa nikihofia kuhusu wewe. Walikupeleka wapi?)” Katie alimuuliza Gibson.
“They planned to take me to Texas but when we arrived Shealbon, five kilometre to Texas, I ascaped? (Walipanga kunipeleka Texas lakini tulipofika Shealbon, kilometa tano kabla ya kuingia Texas, niliwatoroka)” Gibson alijibu.
“How did you escape? (Ulitoroka vipi?)”
“I fought them (Nilipigana nao)
“Sure? (Kweli)
“Yeah” Gibson alijibu.
Waliendelea kuongea zaidi na zaidi huku Katie akishindwa kabisa kuificha furaha yake ambayo alikuwa nayo, muda wote alikuwa pembeni ya mume wake akimkumbatia tu, alishindwa kumuachia, aliona kama angekaa mbali nae kidogo basi angeweza kuondoka mikononi mwake kitu ambacho hakuwa akikitaka kitokee.
Kichwa cha Gibson kilikuwa kikiwaza kitu kingine kabisa, hakuyafikiria mapenzi hata kidogo, kitu ambacho alikuwa akikifikiria sana kwa wakati huo ni fedha ambazo alikuwa ameahidiwa na Daniel kama angefanikiwa kuvunja ndoa yake na mkewe, Katie.
Mpaka kufika kipindi hicho wala hakujua angeanzia wapi, alimuona Katie akiwa na mapenzi ya kweli sana kwake jambo ambalo ilikuwa ni vigumu sana kuufanya uamuzi ule ambao alikuwa ameambiwa kuufanya ndani ya wiki moja. Mapenzi ya Katie ndio ambayo yalikuwa yakimuweka katika hali ngumu ya kuufanya uamuzi ule.
Dhahiri alionekana kuwa katika wakati mgumu kuufanya uamuzi ule lakini kiasi cha fedha ambacho alikuwa ameahidiwa kilikuwa ni kiasi kikubwa sana ambacho angeonekana kuwa mjinga sana kama asingekifanya kile ambacho alikuwa ameambiwa kukifanya.
Usiku, mawazo yake yalikuwa yakimfikiria Daniel na kufikiria kile ambacho alikuwa ameambiwa kukifanya. Japokuwa mke wake, Katie kwa wakati huo alikuwa kwenye wakati mgumu wa kumtaka mume wake wafanye mapenzi lakini kwa Gibson wala mawazo yake hayakuwa yametulia kabisa, hakujisikia kabisa kufanya kitu hicho.
Katie hakutaka kutulia, alikuwa akimpapasapapasa mumewe mpaka pale hamu ya kufanya tendo lile ilipomshika na kuanza kufanya. Kwa kipindi kile, tendo lile wala halikuwa na utamu wowote kwa upande wa Gibson, mawazo yake yalikuwa yakimfikiria Daniel tu, hasa kitita ambacho alikuwa ameahidiwa kukipata pale atakapokamilisha kuvunja mkataba wa ndoa na Katie.
Siku ya kwanza ikakatika, bado Gibson alikuwa kwenye wakati mgumu sana kukamilisha mpango ambao alikuwa ameambiwa na Daniel kuukamilisha. Muda mwingi alikuwa akionekana kuwa mpole, furaha ambayo alikuwa nayo katika kipindi cha nyuma ilikuwa imepotea kabisa.
Katie akaonekana kuwa na wasiwasi, kamwe hakutaka kumuona mume wake akiwa katika hali ya unyonge jambo ambalo alikuwa akimuuliza sana lakini Gibson alikuwa akimficha kwa kumwambia sababu nyingine ambazo wala hazikuwa na maana yoyote ile.
Siku ya pili ilikuwa imekwishakatika na ya tatu kuingia. Bado Gibson alikuwa akiendelea kujiuliza ni sababu gani ambazo angezisema ili kuuvunja mkataba wa ndoa ambao walikuwa wamewekeana katika kipindi walichooana. Kwa Gibson, mambo yalionekana kuwa magumu sana, kila alivyokuwa akimwangalia Katie na kuona jinsi alivyokuwa akimpenda, alijiona kufanya kosa kubwa sana kama angeamua kufanya hivyo.
Siku ya nne ikaingia, ya tano na hatimae wiki nzima kukatika. Bado Gibson alikuwa kwenye wakati mgumu, wasiwasi wa kuuawa tayari ukaanza kumuingia kama ahadi iliyotolewa na Daniel endapo asingeweza kukamilisha kile ambacho alikuwa amemwambia. Siku moja baada ya wiki ilipoingia, akashtukia akipigiwa simu na namba ngeni, alipoipokea, alikuwa Daniel.
“Umefikia wapi?” Sauti ya Daniel ilisikika ikiuliza.
“Bado sijaanza kazi. Nahofia utanigeuka” Gibson alimwambia.
“Kukugeuka! Kivipi?”
“Kama nikikamilisha kufanya ulichoniambia, halafu fedha haujaniingizia, hauoni tatizo hilo?” Gibson alimuuliza.
“Ok! Nakuingizia nusu ya fedha. Utakapokamilisha, nakumalizia” Daniel alimwambia Gibson.
“Hapo utakuwa haupo sawa. Ziingize zote kabisa”
“Sasa nitaingizaje fedha zote na wakati kitu ninachokitaka hakijafanyika?”
“Sasa na mimi nitauvunjaje mkataba wa ndoa na wakati fedha zangu hazijamaliziwa?”
“Ok! Kwa hiyo nikiingiza zote utakamilisha kila kitu?”
“Ndio”
“Sawa. Nakwenda kukuingizia leo hii hii. Na ninataka kazi ifanyike ndani ya masaa ishirini na nne. Umenielewa?” Daniel aliuliza huku sauti yake ikiwa imebadilika na kuwa ya hasira zaidi.
“Nimekuelewa”
Ndani ya masaa mawili, meseji ikaingia ndani ya simu ya Gibson kumtaarifu kwamba kiasi cha dola milioni kumi kilikuwa kimeingizwa ndani ya akaunti yake. Gibson hakuamini kama kweli fedha zile zilikuwa zimekwishaingizwa kwenye akaunti yake. Kazi ilikuwa imebakia moja tu kwa wakati huo, kuuvunja mkataba wa ndoa yake na Katie.
Siku hiyo ofisini hakukukalika hata kidogo, muda wote alikuwa akifikiria ni kwa namna gani angeweza kufanya kile ambacho alikuwa amekipanga kukifanya. Akaanza kupekua katika kabati la mafaili yake na kisha kutoa karatasi kadhaa ambazo zilikuwa zikionyesha ni kiasi gani cha fedha alikuwa amekituma nchini Tanzania.
Tayari yeye binafsi alikuwa amekwishatumia zaidi ya dola elfu sabini nchini Tanzania ambazo zilikuwa sawa na shilingi milioni mia na hamsini. Tayari kwa wakati huo alijiona kuwa na fedha za kutosha na hii ilionekana kutosha kabisa kurudi nchini Tanzania.
“Nitaanzisha timbwili nyumbani” Gibson alisema.
“Yaani leo hakulaliki mpaka mkataba uvunjwe” Gibson alijisemea na kuanza safari ya kuelekea nyumbani.
Siku hiyo alionekana kupania kile ambacho alikuwa amekipanga kukifanya, hakutaka kuendelea kuishi na Katie tena kwa kuwa alikuwa amekwishaingiziwa kiasi kikubwa cha fedha katika akaunti yake. Hakujua ni aina gani ya maumivu ambayo angeyapata Katie, kitu ambacho alikuwa akikijali kwa wakati huo kilikuwa fedha tu.
Alipofika nyumbani, akaegesha gari na kuteremka huku akianza kuelekea ndani. Alichokifanya hapo ni kujifanya kuwa na wasiwasi mkubwa mno kitu ambacho kilionekana kuwashangaza hata wafanyakazi wa ndani. Gibson siku hiyo alionekana kutokujiamini kabisa, alikuwa akionekana kuwa na mashaka makubwa sana usoni mwake.
Hata Katie aliporudi nyumbani hapo, bado Gibson alikuwa akiigiza kuwa katika hali ile ile, hali ya kuwa na mashaka makubwa. Katie alipomuuliza sababu, hakujibu kitu zaidi ya kuendelea kuonekana katika hali ile ile ambayo ilikuwa ikimtia wasiwasi Katie.
“Kuna nini mpenzi?” Katie aliuliza kwa sauti ya unyonge.
“Nimepokea simu ya kifo” Gibson alijibu.
“Simu gani tena?”
“Ya kifo. Nimeambiwa nijiandae kufa. Muda wowote ninauawa kuanzia sasa hivi. Aina ya kifo changu kitakuwa ni kama cha John F. Kennedy, kufyatuliwa risasi kadhaa za kichwa” Gibson alisema huku akionekana kuwa na wasiwasi.
“Hapana mpenzi, hautakiwi kuwa na wasiwasi kabisa. Ngoja niwapigie simu polisi” Katie alimwambia Gibson.
“Hapana mke wangu. Ni lazima niondoke hapa”
“Uondoke? Uelekee wapi tena?”
“Nyumbani, Tanzania”
“Kufanya nini?”
“Nafikiri nitakuwa salama kutoka katika mikono ya watu hawa wanaonitafuta” Gibson alijibu.
“Mbona umechukua uamuzi wa haraka sana?”
“Ndio hivyo mke wangu”
“Kwa hiyo utaniacha mimi mwenyewe? Utakubali kukaa mbali nami?” Katie aliuliza huku akionekana kuwa na wasiwasi.
“Inawezekana. Najua haya yote yanatokea kwa ajili yako, kama ningekuwa nimemuoa mwanamke wa kawaida nadhani haya yote wala yasingenitokea kabisa. Nilitekwa, nikatoroka, leo hii napokea simu ya kifo, nadhani maisha yangu yapo ukingoni kama nitaendelea kuishi katika nchi hii ya ugeni” Gibson alisema.
“Kwa maana hiyo unataka tuachane?” Katie alimuuliza Gibson.
Gibson alibaki kimya, swali ambalo alikuwa ameulizwa likaonekana kuwa gumu kujibika, akayapeleka macho yake usoni mwa Katie, Katie alikuwa amebadilika sana, macho tayari yalikuwa mekundu hali iliyoonyesha kwamba muda wowote ule machozi yangetiririka mashavuni mwake.
“Mbona kimya tena? Kwa maana hiyo unataka tuachane?” Katie alimuuliza tena.
“Kama inawezekana” Gibson alijibu.
“Haiwezekani. Haiwezekani hata kidogo. Hapa mpaka mkataba uishe” Katie alimwambia Gibson maneno ambayo yalionekana kumchanganya.
Kwa haraka sana mawazo yake yakahamia kwa Daniel, tayari kukataa kwa Katie kulionekana kumsababishia kifo kutoka kwa Daniel ambaye alikuwa amekwishamuingizia kiasi kikubwa cha fedha katika akaunti yake. Gibson akaonekana kuchoshwa na jibu la Katie ambaye alianza kulia.
“Kuvunja mkataba wa ndoa. Haiwezekani kabisa” Katie alimwambia Gibson katika kipindi ambacho simu ya Gibson ilikuwa ikiita, alipoichukua na kuiangalia, ilikuwa namba ya Daniel, namba ambayo ilikuwa ikimtia wasiwasi.
“Umefikia wapi?” Daniel alimuuliza Gibson.
“Bado kwanza” Gibson alijibu kwa sauti ya chini ambayo alihakikisha Katie asikii.
“Sawa. Una masaa mawili tu. Usipokamilisha. Tunakuja kukua humo humo ndani” Daniel alimwambia Gibson na kisha kukata simu huku akimwacha Gibson akitokwa na kijasho chembamba kilichojaa wasiwasi.

Je nini kitaendelea?
Je Gibson ataweza kuvunja mkataba wa ndoa na Katie?
Itaendelea kesho usiku

IMEDHAMINIWA NA DICK SOUND,ZANNEL BONGO LADIES WEAR,MAC AUTO ACCOSSERIES na FACEBOOK TAKE AWAY Wauzaji wa chips tamu kinondoni.

No comments:

Post a Comment