Msichana Katie alikuwa akiendelea kufanyakazi zake kama
kawaida huku akionekana kutokuwa na wasiwasi hata kidogo. Muda wote alikuwa bize
akifanya kazi zake lakini huku mawazo yake yakiwa yanamfikiria Gibson. Mapenzi
ambayo alikuwa nayo kwa Gibson yalikuwa makubwa, pengo kubwa ambalo alikuwa nalo
moyoni mwake wala halikuweza kuzibika hata mara moja.
Gibson alikuwa
ameuumiza moyo wake kupita kawaida, muda mwingi alikuwa akionekana mpweke, muda
wote alikuwa akiomba Mungu vijana ambao alikuwa amewatuma nchini Tanzania
wafanye kazi kama ambavyo aliitaka ifanyike. Muda mwingi alikuwa akiwasiliana
nao kwa kutumia mtandao wa simu wa Kimataifa wa Tricom ambao ulikuwa ukitumiwa
sana na wazungu kutoka Marekani na barani Ulaya.
Kila alipokuwa akiwasiliana
nao, aliambiwa kuwa mvumilivu kwa sababu kila kitu kilikuwa kikiendelea kama
kilivyotakiwa kiwe. Katie hakuwa na jinsi, kitu ambacho alikuwa akikifanya kwa
wakati huo ni kuendelea kuwa mvumilivu kama kawaida.
Katie aliendelea kuwa
kwenye lindi la mawazo mpaka kipindi kile ambacho akaanza kupokea maua
mbalimbali ya kimapenzi pamoja na zawadi nyingi zilizokuwa zikihusu mapenzi.
Katie alionekana kushangaa, hakujua ni mtu gani ambaye alikuwa akimtumia zawadi
hizo ambazo zilikuwa zikija mfululizo, yaani asubuhi, mchana na
jioni.
Kutokana na hali ambayo alikuwa nayo katika kipindi hicho wala
hakutaka kujali sana kuhusiana na maua hayo na wala hakutaka kumjua mtu ambaye
alikuwa akimtumia vitu hivyo vyote. Mawazo yake kwa wakati huo yalikuwa
yametulia kwa mtu mmoja tu, mtu ambaye alikuwa amemuachia tundu kubwa moyoni
mwake, tundu ambalo lilikuwa likiendelea kuuma kadri siku zilivyozidi kwenda
mbele.
Zawadi ziliendelea kumiminika nyumbani kwake zaidi na zaidi mpaka
kufikia kipindi ambacho akatamani kumuona mtu huyo ambaye alikuwa akitumia muda
mwingi kumtumia zawadi mbalimbali. Alichokifanya ni kumpigia simu kupitia namba
zake ambazo alikuwa akiziambatisha katika zawadi mbalimbali alizokuwa
akimletea.
Siku iliyofuata, mwanaume huyo, Daniel akafika nyumbani kwa Katie
na moja kwa moja kukaribishwa ndani. Katie hakuonekana kuamini, mwanaume ambaye
alikuwa ameingia ndani ya nyumba yake alikuwa akimfahamu vilivyo, alikuwa
Daniel, mtu ambaye alikuwa mpenzi wake na ndiye alikuwa mtu ambaye aliutoa
usichana wake katika miaka ya nyuma, kipindi ambacho walikuwa wakiishi
mitaani.
Kwa mbali, uso wake ukaanza kuonyesha tabasamu, akaanza kumsogelea
Daniel na kisha kumkumbatia. Hiyo ikaonekana kuwa faraja kwake, kumbatio ambalo
alikuwa amelipata kutoka kwa Daniel likaonekana kumfariji na kumsahaulisha na
Gibson kwa sekunde chache.
Baada ya hapo wakaanza kuongea mambo mengi ya
nyuma ambayo yalikuwa yametokea katika maisha yao katika kipindi ambacho
walikuwa wakiishi mitaani hata kabla ya Katie kujiingiza katika uchezaji wa
filamu za ngono, hatua ambayo ilionekana kumuumiza sana Daniel ambaye alikuwa
kwenye mapenzi mazito na Katie.
Daniel hakutaka kuwa nyuma, nae akaanza
kumuelezea Katie kuhusu maisha yake toka siku ambayo walikuwa wametengana.
Alimuelezea mambo mengi mpaka alivyokwenda nchini Uingereza na kutafuta fedha
kwa nguvu mpaka kufikia hatua ya kuwa tajiri mkubwa. Historia zao zilionekana
kufanana, walianzia maisha ya mitaani, maisha ambayo hayakuwa na ubora kabisa
ila katika muda huo, wote walikuwa matajiri wakubwa.
Daniel hakutaka kukaa
kimya, kwa wakati huo bado alikuwa akiona kwamba kulikuwa na uhitaji mkubwa wa
kuzielezea hisia zake kwa msichana huyo, Katie na kwa jinsi moyo wake ulivyokuwa
umeumia hasa mara baada ya kuona kwamba alikuwa ameolewa na mtu mwingine. Uso wa
Daniel ulionyesha dhahiri kwamba alikuwa ameumizwa sana na tukio lile la ndoa na
hivyo alikuwa akiomba Mungu kila siku kwamba awe tena na Katie kama ilivyokuwa
zamani.
“Unafikiri Mungu amejibu maombi yako?” Katie aliuliza huku
akimwangalia Daniel usoni.
“Yeah! Asilimia mia moja” Daniel alijibu huku
akionekana kujiamini.
“Bado Daniel Itakubidi uombe sana. Unakumbuka kwamba
nilikuacha ingawa ulikuwa kwenye mapenzi nami?” Katie alimuuliza
Daniel.
“Ndio! Nakumbuka”
“Nilikuacha kwa sababu nilitaka kuwa huru zaidi
ya jinsi nilivyokuwa. Sikuwa na fedha, nilikuwa nikishinda hata masaa kumi bila
chakua. Nilitaka kuwa tajiri kama nilivyo kwa sasa. Nitazame sasa, ninaweza kula
chochote ninachotaka, ninaweza kwenda popote ninapotaka kwenda. Nina kila kitu
kwa sasa Daniel” Katie alimwambia Daniel.
“Ninafahamu. Lakini una maana gani
kuniambia hayo yote?” Daniel aliuliza.
“macho yangu” Katie alimwambia
Daniel.
“Ninakupenda Katie” Daniel alimwambia Katie.
“Macho yangu
yanakwambia kila kitu” Katie alimwambia Daniel.
Daniel akasimama pale
alipokuwa amekaa na kisha kuanza kumfuata Katie katika kochi alilokuwa amekaa na
kisha kupiga magoti mbele yake. Tayari macho ya Daniel yalikuwa
yamekwishabadilika, yakaanza kuwa mekundu kwa wakati huo.
Tayari macho ya
Katie yalikuwa yamekwishamueleza kila kitu kwamba kwa wakati huo hakutaka kuwa
nae. Kwa kiasi fulani Daniel akaonekana kuchanganyikiwa, alikuwa ametumia kiasi
kikubwa cha fedha kwa kumtenganisha Katie na Gibson, sasa ingeleta maana gani
kama nae pia asingekuwa na msichana huyo na wakati alikuwa ametoa zaidi ya dola
milioni kumi.
Daniel aliona kwamba kulikuwa na kila sababu ya kulipigania
penzi lake, aliona kwamba kulikuwa na kila sababu ya kumrudisha Katie katika
mikono yake. Hakujali ni kiasi gani cha fedha ambacho angetumia kwa wakati huo,
kitu ambacho alikuwa akikitaka ni kumuona Katie akirudi tena katika mikono yake
kama ilivyokuwa zamani, nyakati zile walizokuwa wakiishi mitaani kama watoto wa
mitaani.
Daniel akamshika Katie mkono huku akimwangalia usoni mwake. Macho ya
Daniel yalikuwa yakionyesha kila dalili kwamba kwa wakati huo alikuwa akimhitaji
sana Katie zaidi ya kitu chochote kile. Alipoona kwamba mguso wake mkono mwa
Katie haukubalisha kitu chochote kile, akaupandisha na kuishika shingo ya Katie
kwa mikono yake miwili.
“Ninakupenda”Daniel alimwambia Katie kwa mara
nyingine tena.
Mawazo ya Katie yakaanza kurudi nyuma, tayari hali ya huruma
ikaonekana kumuingia. Katika maisha yake, hakuwahi kumuona mwanaume akitoa
machozi kwa ajili yake kama ilivyokuwa kwa Daniel katika kipindi hicho. Mawazo
yake ya nyuma ndio ambayo yalikuwa yakiongeza chachu ya kuona kwamba kulikuwa na
kila sababu ya kuwa na mwanaume huyo ambaye kwake alionekana kuwa mvumilivu
kupita kawaida.
“Halikuwa chaguo langu sahihi” Katie alimwambia
Daniel.
“Ninafahamu. Muache aende zake. Sahau kila kitu kuhusu yeye” Daniel
alimwambia Katie.
“Vipi kuhusu kisasi?” Katie aliuliza huku akianza
kulia.
“Hakuna uhitaji wa kufanya hivyo” Daniel alimwambia Katie.
Wote
wakajikuta wakisimama na kisha kukumbatiana. Japokuwa kwa wakati huo lilikuwa
jambo gumu sana kwa Katie kumsahau Gibson lakini akaona kulikuwa na kila sababu
za kumsahau mwanaume huyo na kumuacha Daniel achukue nafasi ndani ya moyo wake.
Mpaka kufikia hatua hiyo, tayari Daniel alikuwa akijiona kuwa mshindi, kiasi
kikubwa cha fedha ambacho alikuwa amekitumia kilionekana kufanya kazi ile ambayo
aliikusudia kufanyika.
Huo ndio ukawa mwanzo wa mahusiano yao ya kimapenzi
kwa mara ya pili tena. Kila mmoja akaanza kumuahidi mwenzake kwamba angempenda
mpaka pale ambapo kifo kingewatenganisha. Hakukuwa na mtu ambaye alikuwa
akifikiria maisha ya baade yangekuwaje baada ya hapo, kitu walichokuwa
wakikifikiria ni kufunga ndoa na kuishi pamoja hapo
baadae.
****
“Unamaanisha mke wangu na mtoto wangu wamekufa” Gibson
aliuliza huku akionekana kutokuamini.
Kila mmoja ndani ya ofisi ile
akaonekana kumshangaa Gibson. Dokta hakuwa ameongea kitu chochote kuhusiana na
mgonjwa wake lakini tayari Gibson akaonekana kufikiria jambo jingine zaidi. Hata
kabla ya kuongea kitu chochote kile, dokta akaanza kuyafikiria maneno ya Gibson.
Alijua na uhakika kwamba mgonjwa ambaye alikuwa ameletwa hospitalini pale ambaye
alitekwa alikuwa mmoja, sasa huyo mtoto alitokea wapi?
Ingawa swali hilo
lilianza kumtatiza kichwani mwake lakini dokta Mnyuzu hakutaka kuuliza kitu
chochote kile zaidi ya kulifungua faili ambalo lilikuwa mezani mwake na kisha
kuanza kuandika vitu fulani ambavyo hakukuwa na mtu yeyote ambaye
alivifahamu.
“Mke wako ni mzima japokuwa hali yake ni mbaya sana” Dokta Myuzu
alimwambia Gibson.
“Imekuwaje tena?”
“Hali inaonyesha kwamba alikuwa
amekabwa kwa kipindi kirefu hali ambayo ilimfanya kutovuta pumzi kwa kiasi
kikubwa, mbaya zaidi, kila alipokuwa akijaribu kuvuta pumzi, hiyo hivyo pumzi
ndogo ambayo ilikuwa ikiingia, ilikuwa ikiingia na vumbi jingi” Dokta Mnyuzu
alimwambia Gibson maneno ambayo yalionekana kumchanganya.
“Kwa hiyo
hatopona?”
“Simaanishi hivyo. Kupona anaweza kupona japokuwa inaweza kuchukua
muda mrefu kwani tumemuwekea mashine ya hewa ya oksijeni ili tuweze kuona
maendeleo yake yatakuwaje?” Dokta Mnyuzu alimwambia Gibson.
“Nakuomba
mponyeni mke wangu. Ninampenda sana, sitaki kumpoteza” Gibson alimwambia dokta
Mnyuzu.
“Hata sisi hatutaki kumpoteza na ndio maana tunajitahidi kufanya kila
tuwezacho kufanya kwa ajili ya kuirudisha afya yake kama ilivyokuwa kabla” Dokta
Mnyuzu alimwambia Gibson.
“Na vipi kuhusu mtoto wangu?” Gibson
aliuliza.
“Mtoto yupi?” Dokta Mnyuzu aliuliza huku akionekana
kushangaa.
“Mtoto wangu, Genuine”
“Sijui kama kuna mtoto aliletwa hapa.
Alikuwa na mkeo?”
“Ndio”
“Hapana. Mwanamke aliletwa peke yake” Dokta
Mnyuzu alimwambia Gibson.
“Sasa mtoto wangu yupo wapi?” Gibson
aliuliza.
“Mmmh! Sijui” Dokta alijibu.
“Kuna kitu nadhani kitakuwa
kimeendelea. Maelezo yote juu ya mtoto tutayapata kutoka kwa wale watekaji”
Manase aliwaambia.
Hawakutaka kuendelea kusubiri ndani ya ofisi ile,
walichokifanya ni kuondoka na kuelekea katika chumba alicholazwa Prisca na kisha
kumuangalia. Prisca alikuwa kimya kitandani, kwa kifupi alikuwa akionekana kama
mtu ambaye tayari alikuwa amekwishakata roho. Gibson akasimama pembeni yake,
tayari macho yake yalikuwa yamekwishaanza kutoa machozi, picha iliyoonekana kwa
mkewe ikaonekana kumuumiza sana.
“Prisca mke wangu! Genuine yupo wapi?”
Gibson alimuuliza Prisca huku machozi yakimtoka japokuwa alikuwa akifahamu
kwamba Prisca asingeweza kujibu kitu chochote kile.
*****
Reuben, Filbert
na Edward walikuwa chini ya ulinzi katika chumba kimoja kidogo huku tayari
mawasiliano yakiwa yamekwishafanyika na makao makuu ya polisi ya jijini Dar es
Salaam na hivyo watu hao walitakiwa kusafirshwa mpaka ndani ya jiji la Dar es
Salaam.
Taratibu zote zilikuwa zimekamilika lakini mpaka muda huo ni kamanda
Manase ndiye alikuwa akisubiriwa kutokana na kuwa na maswali machache na watu
hao. Ilipofika saa kumi na mbili jioni, Manase akaingia katika kituo hicho na
moja kwa moja kuelekea katika chumba kile na kuonana na watekaji wote watatu
ambao walikuwa chini ya ulinzi wa polisi.
Kamanda Manase akaanza kuwaangalia
kwa zamu, alipoona ameridhika, akakiweka chini kiti ambacho alikuwa ameingia
nacho ndani ya chumba kile na kisha kutulia. Kwa wakati huo alikuwa akihitaji
kufahamu kitu kimoja tu, sehemu alipokuwa mtoto Genuine ambaye hadi katika
kipidi hicho hawakuwa wamemuona.
Reuben hakutaka kuficha, akaanza kuelezea
kila kitu kilichokuwa kikihusiana na mtoto Genuine. Ilikuwa ni taarifa ambayo
ilimhuzunisha sana Manase, hakujua namna ambavyo alitakiwa kuifikisha taarifa
ile kwa Gibson ambaye alikuwa akitamani sana kusikia taarifa kuhusu mtoto wake
wa pekee.
Manase hakutaka kukaa sana ndani ya chumba kile, alichokifanya ni
kuanza kuelekea hospitalini ambako akamkuta Gibson akiwa ndani ya chumba kile
huku akiendelea kuongea maneno mengi mbele ya uso wa mke wake japokuwa Prisca
hakuwa amefumbua macho.
“Kuna taarifa nimepewa kuhusu mtoto wako” Manase
alimwambia Gibson ambaye akamsogelea karibu huku akiwa na shauku ya kutaka kujua
zaidi.
“Inasemaje?”
“Njoo nje kwanza” Manase alimwambia Gibson na kisha
wote kuelekea nje.
Manase hakutaka kuficha kitu chochote kwa wakati huo,
akamwambia Gibson kila kitu ambacho aliambiwa na Reuben ndani ya chumba kile.
Gibson akauhisi mwili wake ukifa ganzi, akaanza kutetemeka huku hasira zikianza
kumpanda.
“Unasemaje?”
“Hivyo ndivyo ilivyotokea. Kwa kweli imenihuzunisha
sana. Huu ni unyama mkubwa sana kuwahi kutokea” Manase alimwambia
Gibson.
Hiyo ilikuwa ni taarifa mbaya ambayo iliuumiza moyo wa Gibson kupita
kawaida. Machozi yakaanza kutiririka mashavuni mwa Gibson, kile ambacho alikuwa
amekisikia kiliuchoma sana moyo wake. Akalifuata benchi na kisha kulikalia huku
akikiinamisha kichwa chake chini.
Taswira ya mtoto wake ikaanza kumjia
kichwani, alikumbuka mambo mengi kuhusiana na mtoto wake, akalikumbuka tabasamu
lake, akaanza kukikumbuka kicheko chake hasa pale ambapo alikuwa akimfanyia vitu
ambavyo vilikuwa vikimfanya kucheka.
Katika kila kitu ambacho alikuwa
akikifikiria kwa wakati huo kilikuwa kikizidi kumuumiza moyo wake kupita
kawaida. Mtoto wake ambaye alikuwa akimpenda sana, kwa wakati huo hakuwa pamoja
nae tena, alikuwa ameuawa katika kifo kibaya ambacho kila mtu ambaye angesikia,
angeumia moyoni.
Wakati mwingine, alihisi kuisikia sauti moyoni mwake, sauti
ambayo ilikuwa ikisisitiza kwamba kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea yalikuwa
ni matunda ya vitu ambavyo alikuwa amevipanda kabla. Kwa wakati huo ulikuwa muda
wa mavuno wa yale ambayo alikuwa amepanda siku za nyuma.
Usaliti ambao
alikuwa ameufanya kwa mke wake, Prisca ndio ambao ulikuwa umeleta matatizo yale
yote. Alijua fika kwamba kama asingekuwa amemsaliti mke wake, Prisca basi kwa
wakati huo asingekuwa katika wakati mgumu kama ambavyo alivyokuwa kwa wakati
huo.
“Ila mimi ndiye niliyesababisha haya yote” Gibson alimwambia
Manase.
“Najua. Ila kwa sasa hautakiwi kujilaumu. Kila kilichotokea,
kimetokea” Manase alimwambia Gibson.
“Nafahamu. Ila naamini kama nisingekuwa
nimemsaliti Prisca kipindi cha nyuma, nina uhakika hata jambo hili lisingetokea
kwa sasa. Usaliti wangu umenigharimu sana katika maisha yangu. Usaliti ambao
niliufanya kipindi kile, hizi ndizo athari zake. Ninajuta kumsaliti mke wangu”
Gibson alimwambia Manase ambaye alikuwa kimya kumsikiliza.
“Fedha zilinifanya
nimsaliti mke wangu. Hizi hizi fedha haziwezi kunirudishia mtoto wangu. Huu
umekuwa ni kama msumali wa moto ndani ya moyo wangu, tukio hili limeniachia
kidonda kikubwa moyoni, kidonda ambacho sidhani kama kuna siku kitakuja kupona”
Gibson alimwambia Manase.
“Usijali Gibson. Kila kitu ni mipango ya
Mungu”
“Hapana. Vitu vingine si mipango ya Mungu. Mungu hakupanga nimsaliti
mke wangu, Mungu hakupanga nisafiri kwenda nchini Marekani na kufunga ndoa na
msichana Katie. Hii ilikuwa mipango yangu, tamaa zangu za kutaka fedha ndizo
ambazo zimenifanya niwe katika hali hii kwa sasa” Gibson alimwambia Manase huku
akitokwa na machozi.
“Usilie Gibson. Jikaze. Wewe ni mwanaume” Manase
aliendelea kumbembeleza Gibson.
“Kujikaza ni vigumu sana. Inaniuma sana
kumpoteza mtoto wangu ambaye nilikuwa nikifanya mambo mengi kwa ajili yake.
Inawezekana mtoto wangu angekuwa rais, inawezekana mtoto wangu angekuwa waziri
mkuu. Ndoto zake za kufikia mafanikio zimefutika kwa sababu ya tamaa zangu za
kutamani sana fedha. Nilichokuwa nikikifikiria ni fedha tu, sikutaka kufikiria
ni kitu gani kingetokea baada ya hapo. Moyo wangu unajuta, sijui ni kwa namna
gani nitakuwa nikiishi na mke wangu bila ya kuwa na mtoto wetu. Nadhani yatakuwa
maisha yatakayoniumiza sana, nadhani yatakuwa ni aina ya maisha ambayo
yatanifanya kukosa amani na furaha ndani ya moyo wangu” Gibson alimwambia Manase
ambaye alibaki kimya huku nae akianza kuyafikiria maneno ya Gibson.
Gibson
aliongea maneno mengi tena kwa sauti ya unyonge. Ingawa maneno yalikuwa mengi
lakini hayakuweza kubadilisha kitu chochote kile, ukweli ulibaki vile vile
kwamba Genuine alikuwa ameuawa kinyama.
Kila kitu kikapangwa na kisha baada
ya siku moja safari ya kurudi jijini Dar es Salaam kuanza. Gibson hakutaka
kumuacha mke wake ahudumiwe mkoani Tanga jambo lililompelekea kumsafirisha
kuelekea jijini Dar es Salaam kwa kutumia usafiri wa ndege.
Je nini
kitaendelea Fuatilia sehemu ya mwisho kesho saa MOJA USIKU.
Imedhaminiwa na dick sound,masa celagem.,husein pamba kali,facebook take away,1 ted na zanel bongo ladies wear.
IGIZO JIPYA LINAFATA LA KAHABA TOKA CHINA.
No comments:
Post a Comment