Mhudumu wa mghahawa wa Casannova
ambao ulikuwa katika hoteli ile ile ya Cassanova bado alikuwa akiwahudumia
wateja wake, Reuben, Filbert na Andrew kama kawaida yake. Kila wakati alikuwa
akiitwa na kurudi huku akiwa na vinywaji mbalimbali mikononi mwake.
Hamadi
hakuonekana kuwa na wasiwasi na wateja wale, alikuwa akiendelea kuwahudumia kama
kawaida yake. Hakutaka kuongea nao hata kidogo japokuwa moyo wake ulikuwa na
shauku kubwa ya kutamani kuongea na wazungu.
Wazungu wale kwake walionekana
kuwa tofauti kidogo, walionekana kuwa haraka huku muda mwingi macho yao wakiwa
hawayatulizi sehemu moja. Hamadi hakuonekana kujali sana hali ambayo walikuwa
nao, kitu ambacho alikuwa akiendelea kukifanya ni kuendelea kuwahudumia kama
kawaida tu.
Wateja wote zaidi ya ishirini ambao walikuwa kwenye mghahawa ule
walikuwa wamekwishahudumiwa na wakati huo walikuwa wakiendelea kula kitendo
ambacho kilimfanya Hamadi na wahudumu wengine wa mghahawa ule kutulia pembeni
huku nao wakiangalia televisheni.
Habari ya utekaji ikaanza kutolewa, kila
mhudumu alionekana kuwa na utulivu mkubwa kuangalia televisheni ambayo ilikuwa
imewekwa kituo cha televisheni ya Taifa. Taarifa ile ikaonekana kumshtua kila
mmoja, mtangazaji alikuwa akitangaza kwamba kulikuwa na wazungu watatu ambao
walikuwa wamehusika na utekaji wa mwanamke mmoja na mtoto mmoja ambaye alikuwa
na umri wa takribani mwaka mmoja.
“Watekaji hao wanakisiwa kukimbilia mkoani
Kilimanjaro, Tanga, Arusha au Manyara” Mtangazaji alisema huku akionekana
kutokuwa na uhakika.
Hapo ndipo ambapo Hamadi alipoanza kuwaangalia wazungu
wale ambao walikuwa mezani. Kwanza akaanza kuwahesabu kwamba walikuwa watatu
kama ambavyo mtangazaji alikuwa ametangaza kwenye televisheni, akawaangalia
tena, wawili nywele zao zilikuwa nyeupe na mmoja nywele zake zikuwa nyeusi, nao
wale wazungu walikuwa vile vile.
Kila kitu ambacho kilikuwa kikitangazwa
kuhusiana na watekaji nyara wale, kilikuwa kikifanana sana na wazungu wale ambao
walikuwa wamekaa katika mghahawa ule. Hamadi akashindwa kuvumilia, tayari
alikuwa na uhakika kwamba wale watekaji ambao walikuwa wakizungumziwa kwenye
televisheni walikuwa wale wazungu ambao walikuwa katika mghahawa
ule.
Alichokifanya Hamadi ni kutoka na kuanza kuelekea jikoni. Alipofika
huko, akachomoa simu yake na kuanza kupiga namba za polisi ambazo zilikuwa
zikijulikana sana 911. Simu ikaanza kuita, wala haikuita muda mrefu, ikapokelewa
na sauti nzito ya mwanaume kusikika.
“Karibu katika kitengo cha usalama wa
Taifa” Sauti ile ilisikika.
“Hallow. Naitwa Hamadi hapa, nipo Tanga Mjini
barabara ya kumi na tatu” Hamadi alisema huku akionekana kuwa na
haraka.
“Kuna tukio lolote lile limetokea huko?”
“Ndio. Hapa kwenye
mghahawa nawaona watu watatu ambao taarifa zinasema kwamba wanatafutwa na jeshi
la polisi kwa tukio walilolifanya la utekaji” Hamadi alisema.
“Sawasawa. Wapo
vipi hao watu?”
“Ni wazungu watatu. Wana kila sifa ambazo mtangazaji wa
televisheni alivyotangaza” Hamadi alisema.
“Upo Tanga sehemu
gani?”
“Barabara ya kumi na tatu katika hoteli ya Cassanova hapa. Fanyeni
haraka, naona kama wanataka kuondoka” Hamadi alisema na kisha kukata
simu.
Hamadi akarudi tena ndani ya mghahawa. Reuben na wenzake bado walikuwa
wakiendelea kunywa kama kawaida yao, walichukua dakika mbili tu baada ya Hamadi
kutoka jikoni wakasimama, wakalipia na kuondoka mahali hapo.
Hamadi aliwaona
polisi wakichelewa kufika mahali hapo, alionekana kuwa na shauku ya kuwaona
polisi wakifika hapo, wakiwakamata na kisha kupewa zawadi nono ambayo ilikuwa
imeandaliwa kwa mtu yeyote ambaye angefanikisha kukamatwa kwa watu wale.
Wala
hazikupita dakika nyingi, defender ya polisi ikasimama nje ya mghahawa ule na
kisha polisi kuruka chini kikomandoo na kuelekea ndani ya mghahawa ule ambapo
moja kwa moja wakamhitaji Hamadi.
“Wapo wapi?” Polisi mmoja alimuuliza huku
akiwa ameshika bunduki.
“Wameondoka muda mchache uliopita”
“Unajua
wameelekea wapi?”
“Wameelekea kule upande wa kaskazini”
“Wamekwenda na
gari gani?”
“Starlet nyeusi”
“Sawa. Twende garini tuwafuate” Polisi yule
alisema.
Hamadi hakuwa na wasiwasi, alichokifanya ni kupanda ndani ya
defender ile ambayo ilikuwa na polisi zaidi ya kumi ambao walikuwa na bunduki na
kisha kuanza kuelekea kule gari lile la watekaji lilipoelekea.
Mpaka kufikia
kipindi hicho polisi wakawa na uhakika kwamba watekaji wale walikuwa njiani
kuelekea mpakani mwa nchi ya Tanzania na Kenya, kuingilia ndani yamji wa
Mombasa. Dereva wa defender lile alikuwa akiendesha kwa mwendo wa kasi sana,
mpaka kufika ndani ya dakika ishirini, walikuwa wakiliona gari lile kwa mbele
umbali wa nusu kilometa.
“Watakuwa ndio wenyewe wale. Ongeza kasi dereva”
Polisi ambaye alionekana kuwa kiongozi alimwambia dereva.
Gari likaongezwa
kasi, kila polisi ambaye alikuwa na bunduki akaanza kuikoki bunduki yake. Tayari
muda wa vita ukaonekana kufikia, walitakiwa kupambana kiume mpaka kuona kwamba
wanawaokoa mateka ambao walikuwa wameshikiliwa.
Gari lile la watekaji
likaenda kwa umbali fulani, wakaliona likikata kona upande wa kushoto na kuingia
porini, nao walipofikia eneo lile, wakakata kona na kuingia porini. Tayari mpaka
kufikia kipindi hicho walikuwa na uhakika kwamba watu wale walikuwa watekaji na
kulikuwa na uhakika wa asilimia mia moja kwamba mateka wale bado walikuwa
nao.
Wakaendelea kuelekea kule porini mpaka kufika sehemu ambayo kulikuwa na
gari lile tu. Walipoanza kulisogelea na kulifikia, hakukuwa na mtu yeyote yule
zaidi ya khanga moja tu ambayo alikuwa ameivaa Prisca.
Wakaanza kusogea
mbele zaidi mpaka kufika sehemu ambayo wakaanza kusikika minong’ono ya watu.
Wakajificha na kuanza kuchungulia kule minong’ono ilipokuwa ikitokea, macho yao
yakatua kwa watekaji wale huku Reuben akiwa amemkaba Prisca ambaye alikuwa
akijitahidi kujitoa katika roba ile.
Kila mmoja alijua kwamba ule ndio
ulikuwa mwisho wa Prisca, polisi mmoja ambaye alikuwa akisifika kwa shabaha
akaandaa bunduki yake tayari kwa kuwalenga. Mapolisi walionekana kutokuwa na
wasiwasi hata kidogo, tayari walikwishagundua kwamba watekaji wale wala hawakuwa
na bunduki yoyote ile.
“Mlenge yule aliyemkaba mwanamke yule” Polisi kiongozi
alimwambia.
“Kichwani au wapi?”
“Usimuue. Mlenge kwenye ule mkono
uliomkaba mwanamke”
“Nimekuelewa”
Mlio wa risasi ukasikika mahali hapo,
Reuben akaanza kupiga uyowe mkubwa sana, damu zilikuwa zikimtoka mkononi ambao
ulikuwa umepigwa na risasi. Filbert na Andrew wakaona kwamba tayari kila kitu
kilikuwa kimeharibika, walichokifanya ni kuanza kukimbia.
Polisi yule wa
shabaha wala hakuwa na haraka, alichokifanya ni kuilenga miguu yao, wote
wakajikuta wakianguka chini kama mizigo huku wakilia kama watoto. Hawakutaka
kumuacha Reuben vile vile, nae akapigwa risasi nyingine ya mguu, hawakutaka mtu
yeyote yule atoroke kutoka katika mikono yao.
“Kweli una shabaha”
“Hii
ndio kazi yangu bwana. Hata ungeniambia nilenge jicho, ningelilenga
tu”
Polisi wale wakawasogelea na kisha kuwachukua. Wote walikuwa wakilia kwa
maumivu makali, risasi zile zilikuwa zimepenya miguuni mwao. Baadhi ya polisi
wakaanza kumsogelea Prisca, walipogusa mapigo yake ya moyo, alikuwa akihema kwa
mbali sana.
“Tuondokeni” Kiongozi alisema na kisha wote kuingia ndani ya gari
huku mapolisi watatu wakiingia ndani ya ile Starlet pamoja na Prisca ambaye
alikuwa kimya na safari kuelekea Tanga mjini kuanza.
****
Manase alikuwa
akiendesha gari kwa mwendo wa kasi huku Gibson akiwa pembeni yake. Mawazo ya
Gibson kwa wakati huo hayakuweza kutulia hata kidogo, muda wote alikuwa akiiwaza
familia yake, mke wake, Prisca pamoja na mtoto wake, Genuine.
Akili yake wala
haikutulia hata kidogo, kama kuhuzunika tayari alikuwa amehuzunika sana kiasi
ambacho wakati mwingine alikuwa akishikwa na hasira hata zaidi ya simba
aliyejeruhiwa. Maswali kibao yalikuwa yakijazana kichwani kwake kuhusiana na
watekaji ambao alikuwa na uhakika kwamba walikuwa wametumwa na msichana Katie,
msichana ambaye alikuwa amemuoa na kuachana nae kwa sababu kulikuwa na mtu
mwingine ambaye alikuwa akimhitaji zaidi.
Hakukuwa na mtu ambaye alikuwa
akiongea kitu chochote ndani ya gari, kila mtu alikuwa kimya huku wakionekana
kuifuatilia kwa ukaribu safari hiyo ambayo kwao waliiona kwamba ingezaa matunda
kwa kile kitu ambacho walikuwa wakikifuata.
“Wanasemaje? Wamewakamata?”
Gibson alimuuliza Manase ambaye alikuwa amemaliza kuongea na simu.
“Bado
wanaendelea na upekuzi wa kila gari. Nadhani tunaweza kukutana nao njiani pia”
Manase alimjibu Gibson.
Safari bado ilikuwa ikiendelea kama kawaida tena gari
likiendeshwa kwa mwendo wa kasi sana. Baada ya umbali fulani, wakafika katika
eneo ambalo lilikuwa na watu kadhaa wasiozidi ishirini ambao walikuwa
wamezunguka kitu karibu na kichaka huku mikono yao ikiwa kichwani.
Hawakutaka
kusimama wala kushuhudia ni kitu gani ambacho kilikuwa kikiendelea mahali pale,
walichokifanya ni kuendelea na safari yao huku wakionekana kuwa na haraka kupita
kawaida bila kujua kwamba watu walewalikuwa wameizunguka maiti ya genuine ambaye
alikuwa ametupwa wakati gari likiwa katika mwendo wa kasi. Safari iliendelea
zaidi na zaidi mpaka kufika Segera, hakukuwa na mtekaji yeyote ambaye alikuwa
amekamatwa na polisi wale.
Kila mmoja alionekana kuchanganyikiwa,
hawakuonekana kuelewa mahali ambapo watekaji wale walikuwa wamepitia. Kila mmoja
alionekana kutokuelewa, mpaka kufikia muda huo hawakuwa na uhakika kama watekaji
wale walikuwa wamekwishavuka mahali hapo au bado.
Kadri muda ulivyozidi
kwenda mbele na ndivyo ambavyo walionekana kuchanganyikiwa zaidi, kwanza
hawakutaka kuendelea na safari yao, walichokifanya ni kupaki gari pembeni hapo
Segera na kuanza kuongea kuona nini kilitakiwa kufuata.
“Kwa hiyo tufanye
nini?” Dokta Phillip aliuliza.
“Bado sijajua. Yaani hapa
nimekwishachanganyikiwa kabisa. Sijui hawa watekaji watakuwa wamepita njia gani
na wakati watu kule Chalinze waliwaona wakichukua njia hii” Manase alisema huku
akiitoa simu yake.
Muda wote huo Gibson alikuwa amebaki kimya, kichwa chake
kilikuwa kikiifikiria familia yake tu. Hakujua mahali ambapo watekaji wale
walipokuwa wameichukua familia yake. Muda wote moyo wake ulikuwa ukifahamu
kwamba ni msichana Katie ndiye ambaye alikuwa ameucheza mchezo mzima mpaka
kufikia muda huo.
“Huku hawajafika” Manase aliongea simuni.
“Hawajafika?
Hawajafika vipi na wakati watu wamekamatwa Tanga?” Sauti ya pili
ilisikika.
“Wamekamatwa Tanga?” Manase aliuliza huku akionekana
kushtuka.
Swali lile likamfanya Gibson pamoja na dokta Phillip kumsogelea
Manase ambaye bado alikuwa akiongea na simu kutoka makao makuu ya kituo cha
polisi kilichokuwa jijini Dar es Salaam. Aliongea kwa sekunde kadhaa na kisha
kukata simu.
“Wamekamatwa mkoani Tanga” Manase aliwaambia huku akionekana
kutabasamu.
“Asante Yesu! Na vipi kuhusu familia yangu?” Gibson
aliuliza.
“Hilo sijauliza. Cha msingi twendeni Tanga” Manase
aliwaambia.
Hakukuwa na kitu kingine cha zaidi cha kufanya zaidi ya kuingia
ndani ya gari na safari ya kuelekea Tanga kuanza mara moja. Muda mwingi Gibson
alikuwa akiuliza swali lakini maswali yake hayakuwa na majibu zaidi ya kutakiwa
kusubiria mpaka pale ambapo wangeingia Tanga na kuangalia kama familia yake
ilikuwa salama.
Safari iliendelea kwa muda wa dakika arobaini na tano, wakawa
wamekwishafika Tanga ambako wakaelekea mpaka katika kituo kikubwa cha polisi cha
mkoa huo. Kutokana na kujulikana na mapolisi wenzake, Manase akaingia mpaka
ndani.
“Wapo wapi?” Manase alimuuliza polisi mmoja.
“Wapo
ndani”
“Mateka nao wamepatikana?”
“Kwani walikuwa wangapi?”
“Wawili”
Manase alijibu.
“Ndio. Ila sisi tumefanikiwa kumpata mmoja
tu”
“Yupi?”
“Mwanamke”
“Mliangalia vizuri garini na kuona kwamba
hakukuwa na mtoto?”
“Ndio. Tena gari lao lenyewe tumekuja nalo. Nadhani
tukiwabana watatueleza mtoto yupo wapi” Polisi huyo alimwambia Manase.
“Kwa
hiyo huyo mwanamke yupo wapi?”
“Hospitalini. Kijana mmoja alikuwa akitaka
kumuua kwa kumnyonga shingo. Bahati nzuri shabaha za Shabani zilitusaidia”
Polisi yule alijibu.
“Mmempeleka hospitali gani?”
“Hospitali ya
mkoa”
“Hali yake ilikuwaje?”
“Mbaya. Yaani mbaya sana”
Manase hakutaka
kuendelea kukaa ndani ya chumba kile, alichokifanya kwa wakati huo ni kutoka nje
na kisha kumfuata Gibson ambaye akaanza kumuelezea kile ambacho alikuwa
ameelezewa na polisi aliyekuwa ndani ya chumba kile.
Gibson alionekana
kuchanganyikiwa zaidi, hasira kali dhidi ya watekaji wae ikaonekana kumkaba,
walichokifanya kwa wakati huo ni kuingia ndani ya gari na kisha kuanza kuelekea
hospitalini ambako wala hapakuwa mbali kutoka mahali hapo.
Ndani ya gari bado
Gibson alionekana kuwa na hasira kupita kawaida, chuki juu ya Katie ikaanza
kumuingia moyoni mwake na kuzidi kuongezeka kadri muda ulivyozidi kwenda mbele.
Alimchukia sana Katie, kwake, tayari aliona kwamba kila kitu kilikuwa
kimekwisha, hakuona sababu iiyompelekea Katie kuamua kuwatuma watu kuja nchini
Tanzania kwa ajili ya kuiteka familia yake.
“Nitamuua huyu mwanamke” Gibson
aliwaambia huku akionekana kuwa na hasira za waziwazi.
“Achana nae. Kwanza
tuangalie hali ya mke wako” Manase alimwambia Gibson.
“Sawa! Ila haijalishi
kama atapona au atakufa. Nitamuua tu” Gibson alimwambia.
“Nakushauri uiachie
sheria ili ichukue mkondo wake. Unaweza kujuta hapo baadae kwa kujichukulia
sheria mkononi” Manase alimwambia Gibson ambaye alionekana kutokuelewa
kabisa.
Baada ya dakika chache wakawa wamekwishafika katika hospitali ya mkoa
wa Tanga na kisha kuteremka. Moja kwa moja wakaanza kupiga hatua kuelekea sehemu
ya mapokezi ambako wakajitambulisha na kisha kuelekezwa sehemu ambayo walitakiwa
kuelekea.
“Twendeni kwa dokta mkuu kwanza” Manase aliwaambia.
“Kwa nini
tusielekee kwenye chumba alicholazwa mke wangu na mtoto wangu?” Gibson aliuliza
bila kujua kwamba mtoto wake hakuwepo mahali hapo
“Muda wa kuona wagonjwa
umekwishapita na ndio maana nawaambia twendeni huko ili tuongee nae na
kuturuhusu” Manase aliwaambia.
Hakukuwa na mtu yeyote ambaye alionekana
kupinga, walichokifanya ni kuanza kuelekea katika ofisi ya dokta mkuu na
kukaribishwa. Uso wa Gibson haukuonekana kuwa na furaha kabisa, muda wote
alikuwa akionekana kuwa na majonzi makubwa.
Wakaanza kujitambulisha kwa dokta
Mnyuzu na kisha kutaka kupatiwa maelezo yanayotosheleza kuhusiana na mgonjwa wao
ambaye alikuwa ameletwa ndani ya hospitali ile ya mkoa. Hata kabla ya kuongea
kitu chochote kile, dokta Mnyuzu akakaa kimya kwa muda huku akiwaangali kwa
zamu, aliporidhika, akayagandisha macho yake usoni mwa Gibson.
“Mwanamke yule
ni mke wako?” Dokta Mnyuzu alimuuliza Gibson.
“Ndio” Gibson alijibu.
“Pole
sana. Ni habari mbaya lakini haina budi kukupa. Wewe ni mwanaume, nakuomba
ujikaze kiume” Dokta Mnyuzu alimwambia Gibson ambaye hapo hapo akaonekana
kuishiwa nguvu, akakiegemeza kichwa chake huku akimwangalia Dokta
Mnyuzu.
“Mkeo amefariki” Ilikuwa ni sauti ambayo ilikuwa ikisikika mara kwa
mara kichwani mwa Gibson.
Je nini kitaendelea?
Je Prisca
amekufa?
Je Gibson atafanya nini akisikia hali ya mkewe?
Tusisahau uzinduzi wa video ya majanga jumapili @new maisha club dar.snura atasindikizwa na madee,mirror,ali nipishe,timbulo,baucha na wema sepetu ndio atakaeizindua video ya majanga.
uzinduzi huu umedhaminiwa na DICK SOUND,HUSEIN PAMBA KALI,1 TED,CLOUDS FM,CELAGEM na XTREME DEEJAYZ.usikose.
No comments:
Post a Comment