Gibson alikuwa amekaa ofisini
mwake huku akiendelea kufanya kazi zake kama kawaida. Kwa wakati huo, akili yake
alikuwa ameituliza kwa mke wake tu, hakutaka kumfikiria Katie wala kitu chochote
ambacho kilikuwa kimetokea katika maisha yake pamoja na Katie.
Alikuwa
amekwishaomba msamaha kwa mke wake kwa hiyo wala hakutaka kumkasirisha tena na
wala hakutaka kutembea nje ya ndoa. Moyo wake ulikuwa ukimpenda mke wake zaidi
ya kitu chochote kile katika maisha yake.
Mtoto wao, Genuine alikuwa chachu
kubwa ya mapenzi yao, alimpenda sana mtoto wake na kumthamini sana. Mara kwa
mara alikuwa akitamani kuwa karibu nae, kila alipokuwa akimwangalia Genuine,
alikuwa akiona umuhimu wa kumpenda zaidi mke wake, Prisca.
Gibson aliendelea
kufanya kazi zake kama kawaida. Ilipofika saa nne asubuhi, akaanza kujisikia
hali ya tofauti moyoni mwake. Moyo ukaanza kujaa majonzi huku ukiwa mzito. Hali
hiyo haikuonekana kuwa ya kawaida moyoni mwake, akaacha kufanya kila kitu na
kutulia.
Hali haikuonekana kubadilika, bado alikuwa akiendelea kuihisi hali
ile ile. Amani moyoni mwake ikatoweka, alichokifanya kwa wakati huo ni kuichukua
simu yake na kuanza kuangalia baadhi ya namba, alipoona ameridhika, akampigia
simu mke wake.
“Umefikia wapi?” Gibson alimuuliza Prisca.
“Kuhusu nini
mpenzi?”
“Kumpeleka mtoto hospitalini”
“Ndio najiandaa mpenzi. Nilikuwa
nikimnywesha uji kwanza”
“Sawa. Nisubiri nakuja”
“Vipi kuhusu
kazi?”
“Hakuna tatizo mpenzi. Moyo wangu umekuwa mzito sana kubaki ofisini,
amani imenitoweka kabisa moyoni” Gibson alimwambia Prisca.
“Mmmh! Sasa tatizo
nini?”
“Bado sijajua. Nisubiri nije huko huko. Nitataka kuwa karibu na
familia yangu” Gibson alimwambia Prisca.
“Sawa. Nakusubiri mpenzi” Prisca
alijibu na kisha kukata simu.
Gibson hakutaka kuendelea kubaki ndani ya ifisi
ile, alichokifanya ni kutoka na kisha kuanza kuelekea sehemu ya magari na
kuchukua gari lake na kuanza kuelekea nyumbani kwake. Hali ya moyo wake wala
haikubadilika kabisa, ilikuwa vile vile. Mawazo yalikuwa yakimsonga kichwani
mwake, hakujua ni kitu gani ambacho kilikuwa kikitaka kutokea ambacho mpaka
katika wakati huo kilikuwa kimemkosesha amani kabisa.
“Kuna nini tena? Mbona
najisikia hivi moyoni?” Gibson alikuwa akijiuliza mara kwa mara lakini hakupata
jibu lolote lile.
Kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo hali
ile ilivyozidi zaidi na zaidi, alikuwa akiendesha gari lake lakini akili yake
ilikuwa ikifikiria mambo mengi kwa wakati huo. Alikuwa akizifikiria biashara
zake kwa kuona kwamba labda kungekuwa na kitu kingetokea au aliona dalili fulani
lakini kila alipokuwa akijzifikiria, hakuona jambo lolote lile baya.
Alifika
nyumbani baada ya dakika kumi, kitu cha kwanza ni kuelekea chumbani kwake,
alipokuta mke wake, akamkumbatia kwa furaha. Akaendelea kumuelezea mke wake juu
ya hali ambayo alikuwa nayo moyoni, Prisca ndiye mtu pekee ambaye alikuwa
akimtoa wasiwasi moyoni mwake.
“Usijali mume wangu. Kila kitu kitakuwa salama
tu na wala halitotokea jambo lolote lile baya” Prisca alimwambia Gibson.
“Una
uhakika?”
“Yeah! Hatutakiwi kuogopa kitu chochote kile mpenzi” Prisca
alimuondoa wasiwasi Gibson.
“Ok! Twende huko hospitalini. Leo sitaki kukaa
mbali nanyi kabisa. Ninyi ndio kila kitu kwangu” Gibson alimwambia
Prisca.
Alipomaliza kujiandaa, Prisca na Gibson wakaanza kuelekea garini na
kisha kuanza safari ya kuelekea katika hospitali hapo Masaki. Walitumia dakika
chache sana wakawa wamekwishafika katika hospitali ile ambapo Prisca akaelekea
kujiandikisha na kurudi benchini kwa mumewe.
“Vipi?”
“Nimejiandikisha
tu”
“Kwa hiyo inabidi usubiri hapa kama
wenzako?”
“Ndio”
“Sawa”
Waliendelea kukaa katika lile benchi huku
wanawake wengine wakiendelea kufika mahali pale pamoja na watoto wao. Baada ya
dakika thelathini, zamu ya Prisca ikafika na kuingia ndani ya chumba kile kwa
ajili ya kuhudumiwa huku Gibson akimsubiria benchini.
Dakika ziliendelea
kusonga mbele lakini Prisca hakutoka nje ya chumba kile jambo ambalo lilionekana
kumtia wasiwasi Gibson na kuwakasirisha wanawake wengie ambao walionekana kuwa
na haraka. Gibson akaendelea kuwa mvumilivu, nusu saa ya kwanza ikapita, saa
moja likatimia lakini Prisca hakuweza kutoka ndani ya chumba kile.
Gibson
akaonekana kushikwa na wasiwasi, hakujua ni kitu gani ambacho kilikuwa
kikiendelea ndani ya chumba kile mpaka mke wake kucheleweshwa kutoka namna ile
na wakati wanawake wengine walikuwa wakitumia dakika tano hadi kumi.
Gideon
akasimama na kuanza kuusogelea mlango ule na kisha kutaka kuufungua, mlango
ulikuwa umefungwa kwa ndani. Tayari Gibson akazidi kushikwa na wasiwasi zaidi,
alicokifanya ni kuwasiliana na ofisi ya dokta mkuu ambaye akafika mahali hapo
haraka sana.
Wote wakajaribu kufungua mlango lakini wala haukufunguka. Kila
mmoja alibaki kuwa na maswali juu ya kitu ambacho kilikuwa kikiendelea ndani ya
chumba kile.
“Ngoja nipitie mlango wa nyuma” Dokta kuu, Kimaro alimwambia
Gibson.
“Kuna mlango wa nyuma?” Gibson aliuliza.
“Ndio”
Gibson hakutaka
kumuacha daktari aende peke yake, alichokifanya ni kwenda pamoja nae. Walipofika
nyuma, mlango ulikuwa umefungwa lakini walipojaribu kuufungua, ulifunguka. Kila
mtu akapigwa na mshangao, ndani ya chumba kile hakukuwa na mtu yeyote yule jambo
ambalo lilionekana kumshtua kila mtu.
“Hawapo. Mungu wangu! Mke wangu na
mtoto wangu!” Gibson alisema kwa mshtuko.
*****
Huduma za kuwahudumia
watoto zilikuwa zikiendelea kama kawaida hu wakiwa wamekabidhiwa chumba ambacho
kilikuwa na mlango wa nyuma ambao ulionekana kuwa kama mlango wa tahadhari.
Japokuwa mlango huo ulikuwa haujafunguliwa kwa muda wa miaka mitatu lakini
Reuben akahitaji mlango huo ufunguliwe.
Hakukuwa na daktari ambaye alileta
ubishi wowote ule, mlango ukafunguliwa. Saa nne asubuhi, huduma ya chanjo kwa
watoto ikaanza, wanawake wengi walikuwa wamewaleta watoto wao kwa ajili ya
kufanyiwa chanjo. Walichokifanya Reuben, Filbert na Andrew ni kuwaandikisha
wanawake ambao walikuwa wakiwaleta watoto wao pamoja na majina ya wanaume ambao
walikuwa wamezaa nao.
Hiyo ndio ilionekana kuwa nafasi pekee ambayo
ingewafanya wao kumjua mwanamke ambaye angekuja mahali hapo na kuona kwamba huyu
alikuwa mke wa mtu ambaye walikuwa wakimtafuta, Gibson. Wanawake walizidi
kumiminika hospitalini hapo pamoja na watoto wao ambako moja kwa moja
wakajiandikisha majina yao.
“Is she here? (Yupo hapa?)” Reuben alimuuliza
Filbert ambaye alikuwa akiendelea kuandikisha majina.
“Nope. She ain’t here
(Hapana. Hayupo hapa)” Filbert alijibu.
Bado wanawake walikuwa wakiendelea
zaidi na zaidi kujiandikisha katika kupata huduma za watoto wao kupatiwa chanjo
katika hospitali ile kutoka kwa wazungu ambao walionekana kuja kutoa msaaada
bila kufahamu lengo ambalo lilikuwa limewaleta mahali pale na kujifanya kutoa
huduma hiyo.
Dakika ziliendelea kwenda mbele mpaka pale ambapo Prisca
alipokuja kujiandikisha. Filbert akaonekana kushtuka, hakuamini kwamba hatimae
walikuwa wamempata mtu ambaye walikuwa wakimsubiria kwa kipindi kirefu.
Alichokifanya ni kusimama na kuelekea ndani ya chumba kile cha tiba huku lengo
lake likiwa ni kuongea na wenzake.
“She is here (Yupo hapa)” Filbert
aliwaambia.
“Are you sure? (Una uhakika?)
“100% (Asilimia mia
moja)”
Reuben hakuonekana kuamini, alichokifanya ni kuufungua mlango huku
akijifanya kuwaangalia wanawake ambao walikuwa wamekusanyika katika mabenchi.
Wanawake zaidi ya ishirini walikuwa wamekaa kwenye mabenchi yale huku mwanaume
akiwa mmoja tu, Gibson.
“There she is (Yule pale)” Fibert alimwambia
Reuben.
Tabasamu pana likaonekana usoni mwa Gibson, tayari alikuwa ameyaona
mafanikia makubwa mbele yao, kitendo cha Prisca kufika mahali pale kilionekana
kumfurahisha kupita kawaida. Alikuwa na uhakika wa asilimia mia moja kwamba yule
ndiye alikuwa mke wa mtu ambaye walikuwa wakimsubiria mahali hapo kutokana na
Gibson mwenyewe kuonekana pembeni yake.
Walichokifanya ni kuendelea kutoa
huduma kama kawaida yao. Waliandaa kila kitu, gari ambalo walikuja nalo tayari
walikuwa wamekwishalipeleka nyuma ya chumba kile ili lisiwape usumbufu wowote
wakati wa kutoka katika hospitali hiyo.
Wanawake waliendelea kuingia na
kutoka mpaka pale zamu ya Prisca ilipowadia. Akasimama huku akiwa amembeba mtoto
wake, genuine na kuingia ndani ya chumba kile huku mume wake, Gibson akiwa
amemuacha benchini.
Kitu alichokifanya Reuben wakati Prisca ameingia ndani ni
kumchukua mtoto wake, Daniel na kisha kumvutisha Prisca kitambaa kilichokuwa na
dawa ya usingizi, wala hazikupita hata sekunde kumi, Prisca akapitiwa na
usingizi mzito.
Hakukuwa na muda wa kuchelewa mahali hapo, walichokifanya ni
kumbeba Prisca pamoja na mtoto wake na kisha kuanza kuelekea nae nje ambako
wakawaingiza ndani ya gari. Kila kitendo ambacho kilikuwa kikiendelea mahali
hapo, hakukuwa na mtu ambaye alikuwa akikiona kutokana na lile gari kupakiwa
nyumba kabisa ya chumba kile, mahali ambapo si watu wengi walikuwa wakifika mara
kwa mara.
“What next? (Nini kinafuata?)” Andrew aliuliza.
“Lets get out of
here (Tuondokeni mahali hapa)” Reuben aliwaambia na kisha Andrew kuwasha gari
lile.
Andrew hakutaka kuendesha gari kwa mwendo wa kasi kwa kuogopa
kushtukiwa, alichokifanya ni kuendesha gari kwa mwendo wa taratibu na kutoka nje
ya hospitali ile huku kukiwa hakuna hata mtu mmoja ambaye alikuwa akifahamu kitu
ambacho kilikuwa kikiendelea mahali pale.
Safari ambayo walikuwa wameipanga
kwa wakati huo ilikuwa ni kuondoka na kuelekea Tanga ambako huko wangeumuua
Prisca porini na kuunganisha safari yao kuelekea Mombasa na kisha kuelekea
Nairobi ambako wangepanda ndege na kuelekea nchini Marekani huku wakiwa
wamekwishakamilisha kila kitu walichokuwa wameambiwa wakamilishe nchini
Tanzania.
Je nini kitaendelea?
Je Reuben na wenzake wataweza kumuua
Prisca kama walivyopanga?
Je watekaji wataweza kukamatwa?
Itaendelea saa
moja kamili usiku.
Usikose.
No comments:
Post a Comment